Magaidi Waisraeli wanashambulia shule za Wapalestina
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani vikali vitendo vya kigaidi vya hivi punde zaidi vya walowezi wa Israel dhidi ya shule mbili za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Wizara hiyo ilitoa taarifa ya Jumapili ikilaani vikali ugaidi huo baada ya shule mbili za Mabedui wa Kipalestina za Ras al-Tin na al-Tahadi, zote zikiwa mashariki mwa mji wa Ramallah wa Ukingo wa Magharibi, kushambuliwa na makundi ya magaidi walowezi wa Israel.
Wizara hiyo imesema katika taarifa hiyo kwamba, ugaidi huo dhidi ya shule za Wapalestina umetimia katika mfumo wa kile ambacho kimekuwa tabia ya walowezi na 'magenge yao ya kigaidi.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, vitendo hivyo vya kigaidi dhidi ya shule za Wapalestina na wanafunzi wao ni matokeo ya misimamo ya kufurutu ada na matamshi ya mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia wa utawala wa sasa wa Israel, Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich ambao wanawapa ulinzi walowezi hao na makundi yao ya kigaidi.
Wizara hiyo imesema kuwa mashambulizi ya Jumapili dhidi ya shule mbili za Palestina, moja kati ya hizo ikiwa tayari iko kwenye orodha ya ubomoaji wa utawala huo ghasibu, yalifanywa chini ya ulinzi wa moja kwa moja na uungaji mkono wa vikosi vya utawala haramu Israel.
Pia imeshutumu mashambulizi hayo kama "kuongezeka vibaya kwa mashambulio ya walowezi dhidi ya taasisi za elimu za Palestina."
Wizara hiyo imesisitiza kuwa mashambulizi hayo ni sehemu ya majaribio ya Israel ya Kuyahudisha na kupora zaidi ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kupambana na aina zote za kuwepo kwa taifa la Palestina katika maeneo hayo yanayolengwa kuwa makaazi ya walowezi.
Tamko hilo limesema utawala ghasibu wa Israel unabebe dhima ya kulengwa taasisi za elimu za Palestina, na kuitaka jumuiya ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na taasisi yake ya elimu na utamaduni, UNESCO, kutekeleza majukumu yao ya kulinda taasisi za elimu za Palestina.
Israel iliikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi katika vita vilivyoungwa mkono na nchi za Magharibi mwaka 1967, na imekuwa ikijenga makazi haramu ya walowezi wa Kizayuni tangu wakati huo.
Mamia ya maelfu ya walowezi hao wa Kizayuni wanaishi katika vitongoji zaidi ya 230 vilivyojengwa katika eneo hilo la Wapalestina lililoporwa. Wanachi wa Palestina wanasisitiza kuwa eneo hilo lazima liwe sehemu ya taifa lao huru la baadaye.
Jumuiya nzima ya kimataifa inayaona makaazi ya walowezi hao Waisraeli kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa na Mikataba ya Geneva kutokana na ujenzi wake katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu.