Mash'al: Israel imedhamiria kuwafukuza Wapalestina wote wa Ufukwe wa Magharibi
Khalid Mash'al, Kiongozi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS nje ya Palestina amesema, kulingana na fikra za Uzayuni, Wapalestina hawana nafasi yoyote ndani ya ardhi hiyo na inapasa wahamishiwe Jordan.
Baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni, ndilo baraza la mawaziri lililokithiri zaidi katika ufanyaji jinai katika historia ya utawala huo na limedhamiria kuhitimisha kwa manufaa yake mapigano katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds inayokaliwa kwa mabavu na Msikiti wa al-Aqsa.
Kwa mujibu wa gazeti la Rai Al-Yaum, Mash'al amesisitiza kuwa, "uhalisia wa fikra za Uzayuni ni kwamba watu wa Palestina hawana ardhi ya asili. Israel inataka kuulenga Umma wa Kiislamu na hasa Palestina na Jordan na imedhamiria kuwaondoa wakazi wa Ukingo wa Magharibi".
Kiongozi huyo wa Hamas amezungumzia pia njama za Wazayuni za kujaribu kuuyahudisha mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na kuudhibiti kisiasa na kidini mji huo, na akabainisha kuwa, leo msikiti wa Al-Aqsa unakabiliwa na hatari kubwa na unakaribia kubomolewa. Iwapo ardhi, Quds na Al-Aqsa zitatoweka, hakuna kitakachobakia.
Mash'al amezitaka nchi za Kiislamu na Kiarabu zisimame dhidi ya mradi huo wa Uzayuni na akaongezea kwa kusema: "sababu ni kwamba adui amebadilisha vita, hivyo nasi pia inapasa tuvibadilishe. Hivi ni vita vya heshima, dini, Uislamu na hatima".
Kabla ya hapo, Ismail Haniya, Mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas alisema kuwa, baraza la mawaziri la sasa la Wazayuni watenda jinai ni hatari kubwa kwa kadhia ya Palestina, na inapasa kujiandaa barabara kwa ajili ya kukabiliana na njama zake.../