UN: Vitongoji vyote vya Wazayuni Ukingo wa Magharibi ni vitongoji haramu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101334-un_vitongoji_vyote_vya_wazayuni_ukingo_wa_magharibi_ni_vitongoji_haramu
Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani wa "Mashariki ya Kati" amesema kuwa, vitongoji vyote vilivyojengwa na Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina ni haramu na havitambuliwi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 21, 2023 23:06 UTC
  • UN: Vitongoji vyote vya Wazayuni Ukingo wa Magharibi ni vitongoji haramu

Mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika mchakato wa amani wa "Mashariki ya Kati" amesema kuwa, vitongoji vyote vilivyojengwa na Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina ni haramu na havitambuliwi.

Tor Wennesland amenukuliwa na shirika la habari la FARS akisema hayo jana Jumatatu na kuulaumu utawala wa Kizayuni kwa kuendelea kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Nayo televisheni ya Aljazeera ya Qatar imemnukuu Wennesland akisema kuwa, vitongoji vyote vilivyojengwa na Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni vitongoji haramu na ni kikwazo katika kupatikana usalama na amani ya kudumu kwenye eneo hilo. 

Amesema, jitihada za kimataifa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Palesitna zinakwamishwa na hatua hizo za Israel za kupora na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina.

Watoto wa Palesina ni wahanga wakuu wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Afisa huyo amesema pia kuwa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Wapalestina UNRWA hivi sasa linahitajia msaada wa dharura wa dola milioni 35 kwa ajili ya kuwadhaminia chakula Wapalestina milioni moja la laki mbili wanaohitajia mno msaada huo.

Hayo yamekuja katika hali ambayo hivi karibuni viongozi wa utawala wa Kizayuni walikuwa na mazungumzo na viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina inayoongozwa na Mahmoud Abbas.

Kikao hicho kilifanyika katika mji wa Sharm Sheikh nchini Misri na kama kawaida, Israel iliendelea kutoa ahadi chapwa na zisizo na dhamana yoyote ya kutekelezwa. Miongoni mwa ahadi zilizotolewa na Wazayuni ni kusimamisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kuacha kuwashambulia wananchi wa Palestina wakati ambapo hakuna hata siku moja inayopita bila ya Israel kuwashambulia Wapalestina, kuwapora ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.