Umoja wa Ulaya walaani vikali matamshi ya waziri wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101486-umoja_wa_ulaya_walaani_vikali_matamshi_ya_waziri_wa_israel
Umoja wa Ulaya umelaani vikali matamshi yaliyotolewa na waziri mwenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na uhuru wa harakati za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 25, 2023 23:28 UTC
  • Itamar Ben-Gvir
    Itamar Ben-Gvir

Umoja wa Ulaya umelaani vikali matamshi yaliyotolewa na waziri mwenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusiana na uhuru wa harakati za Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Ni baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Itamar Ben-Gvir,  kusema kuwa haki ya yeye, mke wake na watoto wake na hata walowezi wa Kizayuni ya kusafiri salama katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu ni muhimu zaidi kuliko haki ya Wapalestina ya kufanya harakati, na kwamba haki yake ya kuishi inapewa kipaumbele juu ya haki ya Wapalestina kutembea na kufanya harakati katika ardhi yao wenyewe.

kufuatia matamshi hayo ya kibaguzi, Umoja wa Ulaya jana Ijumaa ulitoa taarifa ukilaani vikali matamshi ya Waziri wa Usalama wa Ndani wa utawala wa Kizayuni, Itamar Ben-Gvir, kuhusiana na uhuru wa kufanya harakati wa Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kutangaza kuwa: "Uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israeli lazima uwe na msingi wa kuheshimu haki za binadamu na kaida za kidemokrasia. Binadamu wote ni sawa na wanapaswa kutendewa sawa."

Umoja wa Ulaya kwa mara nyingine tena umesisitiza upinzani wake mkubwa dhidi ya sera za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na hatua za Wazayuni katika uwanja huu, ikiwa ni pamoja na kutatiza na kuzuia harakati ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kusema kwamba, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina ni kinyume cha sheria na ni kikwazo cha kurejeshwa amani.

Umoja wa Ulaya umeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uruhusu na kuboresha uhuru wa harakati za Wapalestina, kuwaruhusu kujenga nyumba na kustawisha uchumi na masuala yao ya kijamii katika maeneo yao.