Hamas yaionya vikali Israel kwamba itashindwa vibaya ikianzisha vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i101560-hamas_yaionya_vikali_israel_kwamba_itashindwa_vibaya_ikianzisha_vita
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa "utashindwa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa" iwapo utaanzisha "vita vya pande zote" katika eneo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2023 01:26 UTC
  • Hamas yaionya vikali Israel kwamba itashindwa vibaya ikianzisha vita

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeuonya vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa "utashindwa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa" iwapo utaanzisha "vita vya pande zote" katika eneo.

Katika mahojiano maalum na mtandao wa habari wa televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon, Saleh al-Arouri, naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, amesema kwamba viongozi wa utawala ghasibu wa Israel unaoongozwa na ubaguzi wa rangi na ufashisti, "watasababisha vita vya kila upande katika eneo” ikiwa watasonga mbele na sera zao za kufurutu ada na zenye msimamo mkali.

Afisa huyo wa Hamas ametangaza kuwa muungano wa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina ziko tayari kuungana ili kushiriki katika vita vya kikanda, na kuongeza kuwa pande zinazohusika ziko tayari na zimejiandaa kwa hilo.

Afisa huyo wa Hamas pia ametoa wito kwa vijana wote wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kushiriki katika harakati za kupigania ukombozi  "kwa njia yoyote inayowezekana."

Pia amegusia majaribio yaliyoshindwa ya Israeli katika Kuyahudisha Ukingo wa Magharibi na kuwatimua Wapalestina.

Ameongeza kuwa baraza la mawaziri la mrengo wa kulia wa Israel la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu linalenga kuwaondoa Wapalestina kutoka Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, kuongeza makaazi haramu ya walowezi wa Kizayuni na kupata udhibiti wa Msikiti wa al-Aqsa.

Saleh al-Arouri

Hayo yanajiri wakati ambao Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni ametoa vitisho vya kumuua Saleh al-Arouri na kukiri pia kwamba sasa hivi utawala huo unapitia kipindi kigumu.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Motomoto za Palestina, Netanyahu amekiri kuwa mhimili wa Muqawama umeuzunguka kitaarifa utawala huo kwa ndani na nje na hivi sasa unakabiliana nao.

Akizungumzia ongezeko la mashambulizi dhidi ya Wazayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Al Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, Netanyahu ameshikilia kuwa Saleh al-Arouri, naibu mkuu wa ofisi ya kisiasa ya harakati ya Hamas na kiongozi wa harakati hiyo ya Muqawama katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ndiye msababishaji wa hali hiyo na kutishia kuwa watamuua.