Haniya: Israel inabeba dhima ya mauaji katika jamii ya Waarabu
(last modified Sun, 03 Sep 2023 07:23:17 GMT )
Sep 03, 2023 07:23 UTC
  • Haniya: Israel inabeba dhima ya mauaji katika jamii ya Waarabu

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema utawala haramu wa Israel unabeba dhima ya mauaji ya kiholela katika jamii ya Waarabu katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumamosi, Ismail Haniya ameulekezea kidole cha lawama utawala wa Tel Aviv na taasisi zake za kijasusi kwa ongezeko la mauaji miongoni mwa Waarabu katika ardhi zilizoghusubiwa.

Haniya amesema bayana kuwa, "Tunaubebesha dhima utawala ghasibu wa Kizayuni kwa umwagaji damu na mauaji yaliyoshtadi ndani ya ardhi (zinazokaliwa kwa mabavu) tokea 1948." 

Kiongozi huyo wa muqawama amesisitiza kuwa, taifa la Palestina halina njia nyingine ya kujikomboa na kuwatimua wavamizi isipokuwa kuendeleza muqawama, uthabiti, mapigano na kuwa na umoja.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya HAMAS amebainisha kuwa: Vyombo vya usalama vya adui Mzayuni vimechukua hatua hatari inayolenga kuwashughulisha watu wetu katika mambo mengine, ili wasahau uhusiano wao wa kidini na kihistoria na Wapalestina wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na walioko uhamishoni.

Sheikh Sami Abed al-Latif, Imam wa Msikiti wa Quba aliyeuawa shahidi

Mapema jana Jumamosi, Sheikh Sami Abed al-Latif, Imam wa Msikiti wa Quba katika mji wa Waarabu wa Kafr Qara huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu aliuawa shahidi kwa kupigwa risasi.

Hii ni katika hali ambayo, msomi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 60, alitambulika sana katika juhudi zake za kujaribu kutatua migogoro katika mji huo wa Waarabu kwa njia za amani.

Tags