Russia: Mazungumzo ya Wayemeni yaendelee
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10210-russia_mazungumzo_ya_wayemeni_yaendelee
Russia imeyataka makundi ya Wayemeni na pande husika katika mgogoro wa nchi hiyo kuunga mkono mazungumzo ya sasa ya Wayemeni yanayoendelea huko Kuwait.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 29, 2016 03:01 UTC
  • Russia: Mazungumzo ya Wayemeni yaendelee

Russia imeyataka makundi ya Wayemeni na pande husika katika mgogoro wa nchi hiyo kuunga mkono mazungumzo ya sasa ya Wayemeni yanayoendelea huko Kuwait.

Taarifa kutoka Moscow zinaeleza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeyataka makundi ya Wayemeni na pande husika katika mgogoro wa nchi hiyo kuzidisha juhudi ili kupata ufumbuzi wa kisiasa wa mgogoro wa nchi yao katika fremu ya mazungumzo yanayoendelea sasa huko Kuwait yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema inatumai kuwa Wayemeni wataweza kuvuka marhala ya hitilafu kuu zinazowakabili sasa na kufikia mapatano kuhusu ramani ya njia iliyopendekezwa na Ismail Ould Sheikh Ahmad Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeongeza kuwa miripuko ya kigaidi iliyotokea hivi karibuni kwenye bandari ya Makala kusini mwa Yemen inathibitisha kushadidi hujuma za kigaidi za kundi la Daesh (ISIS). Russia imesema kuwa kuendelea mapigano ya umwagaji damu huko Yemen kunakwamisha jitihada za kutekelezwa oparesheni dhidi ya ugaidi.