Iraq yasema itafungamana na makubaliano yake ya usalama na Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein, ameihakikishia Iran kuwa nchi yake inasalia na dhamira ya dhati katika kufungamana na makubaliano yake ya kiusalama na Jamhuri ya Kiislamu kuhusu kuyafurusha makundi ya kigaidi yanayoipinga Iran katika eneo la Kurdistan lenye mamlaka ya ndani.
Hussein aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari pamoja na mwenzake wa Austria Alexander Schallenberg katika mji mkuu wa Iraq wa Baghdad siku ya Jumanne.
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iraq alitangaza kuwa: "Tumechukua hatua zinazohitajika kuondoa vikundi vyenye silaha kutoka maeneo ya mpaka kati ya Iraq na Iran. Na kwa ajili hiyo, nitasafiri Jumatano Tehran kufanya mazungumzo na serikali ya Iran kuhusu suala hilo."
Aliongeza, "Katiba yetu hairuhusu ardhi ya Iraqi kutumika kama njia ya kutekeleza mashambulizi dhidi ya nchi jirani. Wakati huo huo, hatukubali mamlaka ya kujitawala kitaifa Iraq kuhujumiwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq pia aliutaja uhusiano wa Iran na Iraq kuwa wenye nguvu na wenye mizizi mirefu.
Amesisitiza kuwa, Iraq haitaruhusu eneo lake kutumiwa na baadhi ya makundi kushambulia Iran.
Matamshi hayo yamekuja siku moja baada ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan’ani kusema makataa iliyotolewa kwa Iraq ya kuyapokonya silaha makundi yanayoipinga Iran yaliyoko katika utawala wa Kurdistan hayatarefushwa.
Kan’ani alisema katika mkutano wa vyombo vya habari vya kila wiki siku ya Jumatatu kwamba: "Msimamo wa Iran uko wazi kabisa. Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Iraq, makataa ya mwisho ya kuyapokonya silaha makundi ya kigaidi na ya wanaotaka kujitenga katika eneo la Kurdistan nchini Iraq inakamilika Septemba 19 na muda huo hautaongezwa kwa njia yoyote ile."
Amebainisha kuwa serikali ya Iraq imechukua hatua kuhusiana na suala hilo na kusisitiza kuwa itatekeleza ahadi zake.
Siku ya Jumatatu pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alionya kwamba kuwepo magaidi katika eneo la Kurdistan ya Iraq ni kinyume na uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa hayo mawili na ni kinyume na Katiba ya Iraq.