Bahrain yaendeleza jinai zake, yawafunga maisha jela watu 8
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i10234-bahrain_yaendeleza_jinai_zake_yawafunga_maisha_jela_watu_8
Katika muendelezo wa wimbi la ukandamizaji na hukumu zisizo za kiadilifu zinazotolewa na utawala wa Manamana dhidi ya wanaharakati na wapinzani, mahakama moja nchini Bahrain imewahukumu kifungo cha maisha jela, wanaharakati wanane wa Kishia wa nchi hiyo sambamba na kuwapokonya uraia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 29, 2016 08:48 UTC
  • Bahrain yaendeleza jinai zake, yawafunga maisha jela watu 8

Katika muendelezo wa wimbi la ukandamizaji na hukumu zisizo za kiadilifu zinazotolewa na utawala wa Manamana dhidi ya wanaharakati na wapinzani, mahakama moja nchini Bahrain imewahukumu kifungo cha maisha jela, wanaharakati wanane wa Kishia wa nchi hiyo sambamba na kuwapokonya uraia.

Duru za mahakama zimearifu kuwa, wanane hao wamehukumiwa kifungo cha miaka minane jela mbali na kuvuliwa uraia wa nchi hiyo, kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya Iran na eti kujiunga na kundi la kigaidi linalotishia usalama wa taifa. Hukumu ya leo Jumatano inajiri katika hali ambayo, hatua ya utawala wa Bahrain kumvua uraia mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim, imeendelea kupokea wimbi la malalamiko na maandamano kutoka jamii ya kimataifa. Kwa mujibu wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Bahrain, watu zaidi ya 260 wamepokonywa uraia na utawala wa Aal-Khalifa tangu mwaka 2012 hadi sasa.

Tovuti ya Mitaala ya Jela (Prison Studies) imetangaza kuwa hadi mwezi Disemba mwaka 2013 utawala wa Bahrain ulikuwa umewafunga jela raia 4,030 ambayo ni idadi kubwa zaidi katika nchi za Mashariki ya Kati kulingana na idadi ya raia wote wa nchi hiyo. Chama kikuu cha upinzani nchini humo cha al-Wefaq karibuni hivi kilitoa ripoti iliyosema kuwa, vyombo vya usalama vya Bahrain vimekamata watu 1,765 wakiwemo watoto wadogo 120 tokea mwaka jana 2015 hadi sasa, kwa lengo la kukandamiza maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga dhulma za utawala wa Manama. Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano tokea Februari mwaka 2011, kushinikiza kung'atuka uongozini utawala wa kifalme wa Aal-Khalifa.