Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti wa al-Aqswa
(last modified Tue, 19 Sep 2023 02:31:45 GMT )
Sep 19, 2023 02:31 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti wa al-Aqswa

Sambamba na maadhimisho ya sikukuu za Kiyahudi, makumi ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wameuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqswa na kufanya vitendo vya kichochezi.

Walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali walivamia msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.

Msikiti wa al-Aqswa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Kipalestina wa eneo takatifu la Quds na utawala wa Israel unajaribu kuharibu utambulisho huo, lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufedhehesha utawala huo wa Kizayuni na kupelekea njama zake kushindwa.

Vitendo vya hujuma za walowezi wa Kizayuni dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vimekithiri zaidi baada ya kuingia madarakani serikali yenye misimamo mikali ya Benjamin Netanyahu ambayo imekuwa ikionyesha chuki za wazi wazi dhidi ya Wapalestina na maeneo yao matakatifu.

Walowezi wa Kizayuni baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikitii wa al-Aqswa

 

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Tangu serikali ya Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu ishike tena hatamu za uongozi, huko Israel, hujuma na uvamizi wa mara kwa mara wa walowezi wa Kizayuni umechukua mkondo mpana zaidi.