Iran: Hotuba ya Netanyahu katika UN inashabihiana na 'onyesho la vichekesho'
Ujumbe wa kidiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa umepuuzilia mbali madai yasiyo na msingi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Israel Benjamin Netanyahu na kusema ni "maonesho ya vichekesho" dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na shughuli zake za kieneo katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa Iran ulisema hayo katika taarifa yake siku ya Jumamosi baada ya Netanyahu kuzungumzia "laana ya Iran ya nyuklia" wakati wa hotuba yake katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huku akidai kuwa eti Iran inatumia "mabilioni ya fedha kuwapa silaha washirika wake wa kigaidi."
Aidha Ujumbe wa Iran katika umeongeza kwamba: "Tuhuma zisizo na msingi zinazotolewa na maafisa wa Israel hazimhadai mtu yeyote tena. Kampeni za chuki dhidi ya Iran na usambazaji wa taarifa potofu na madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran daima imekuwa moja ya vipengele vikuu vya matamshi—au bora kusema, maonyesho ya vichekesho—yanayotolewa na wakuu wa Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa".
Halikadhalika taarifa hiyo ya Iran imesema: "Utawala (wa Israel) unajaribu kuonyesha uwezo wa silaha wa kawaida wa Iran au mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani pekee, ambao uko chini ya ukaguzi mkali zaidi duniani wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, kama changamoto kwa utulivu wa kikanda. Mbinu hii ni hatua ya kinafiki ya kupotosha umma kuhusu hatari halisi inayoletwa na utawala huu kwa amani na usalama wa kikanda, hususan maghala yake ya silaha za nyuklia, mitambo na shughuli za nyuklia ambayo haizingatii usalama.”
Taarifa ya Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesisitiza kuwa, utawala ghasibu wa Israel una rekodi chafu na ndefu ya kuhifadhi, kulinda, na kuipa silaha mitandao hatari zaidi ya kigaidi.
Pia Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umesema: "Utawala vamizi wa Israel umeleta migogoro mingi na ukosefu wa utulivu katika eneo lote. Kwa hivyo, inashangaza kwamba waziri mkuu wa utawala wa Israel alizungumza kuhusu kuendeleza mpango wa amani wa kieneo huku utawala wake wa umwagaji damu ukipanga kunyakua hata maeneo mengi zaidi ya Palestina ambayo tayari yamekaliwa kwa mabavu."