JPPI: Kasi ya Wazayuni kukimbia ardhi za Palestina inaongezeka
Matokeo ya uchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa, kumekuwapo ongezeko kubwa la maombi ya viza kwa Wazayuni na Mayahudi kuhama kutoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Taasisi ya Sera ya Kiyahudi (JPPI) unaonyesha kuwa, asilimia 37 ya Mayahudi wanafikiria kupata hati ya kusafiria na kuondoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina iwapo muswada wenye utata wa "mageuzi ya mahakama" utaidhinishwa na baraza la mawaziri la Israel.
Taasisi ya JPPI imetangaza katika kura hiyo ya maoni kwamba asilimia 32 ya Wazayuni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu wanajisikia vibaya na hawaridhishwi na hali zao.
Katika miezi michache iliyopita, makumi ya miji kutoka kaskazini hadi kusini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, iliyopachikwa jina la Israel, ikiwa ni pamoja na Tel Aviv, Haifa, Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu, Beersheba, Rishon LeZion na Herzliya, imekuwa uwanja wa maandamano dhidi ya baraza la mawaziri la mrengo wa kulia la Benjamin Netanyahu na muswada wa marekebisho na mahakama.
Vinara wa upinzani wa utawala wa Kizayuni wanautambua muswada wa mabadiliko ya mahakama wa baraza la mawaziri la Netanyahu kuwa ni jitihada kudhoofisha mfumo wa mahakama na jaribio la kiongozi huyo la kuzuia kupandishwa kwake kizimbani kutokana na kesi tatu za ufisadi na hongo zinazomkabili. Wanasema kuwa hatua hizo za baraza la mawaziri zinauelekeza utawala huo upande wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na hatimaye kusambaratika.