HAMAS yataka kuendelezwa muqawama dhidi ya Wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesema kuna haja ya kuendeleza muqawama na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
HAMAS imenukuliwa ikisema hayo na shirika la habari la Shahab la Palestina kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 23 ya Intifadha ya al-Aqsa na kueleza kuwa: Muqawama ndilo chaguo letu la pekee la kupata haki zetu.
Harakati hiyo ya muqawama imesisitiza kuwa: Mapambano kwa nguvu zote ndilo chaguo la kistratajia la watu wetu la kupata haki, na kukomboa ardhi na maeneo yetu matakatifu, ukiwemo mji mtukufu wa Quds na Msikiti wa al-Aqsa.
HAMAS imesema hayo katika hali ambayo, walowezi wengi wa Kizayuni wenye misimamo mikali mara kwa mara wamekuwa wakivamia msikiti wa al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi huku wakiwa wanapatiwa ulinzi na vikosi vya usalama vya utawala haramu wa Israel.
Harakati ya HAMAS imesisitiza kuwa: Masjidul Aqsa itasalia kuwa milki na wakfu wa Waislamu; na utawala fashisti wa Kizayuni hauna ustahiki wala mamlaka yoyote juu ya eneo lololote la Msikiti huo mtakatifu.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.