Syria yafungua tena ubalozi wake mjini Riyadh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i102940-syria_yafungua_tena_ubalozi_wake_mjini_riyadh
Ubalozi wa Syria mjini Riyadh umefunguliwa tena huku ujumbe wa wanadiplomasia wa Syria ukirejea Saudi Arabia, vyanzo vya habari vimeripoti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2023 23:01 UTC
  • Syria yafungua tena ubalozi wake mjini Riyadh

Ubalozi wa Syria mjini Riyadh umefunguliwa tena huku ujumbe wa wanadiplomasia wa Syria ukirejea Saudi Arabia, vyanzo vya habari vimeripoti.

Kwa kurejea kwa ujumbe wa kidiplomasia wa Syria nchini Saudi Arabia, ubalozi wa nchi hiyo mjini Riyadh umefunguliwa tena na hivyo kuhhuisha tena uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

Chanzo cha habari cha serikali ya Syria kimeripoti kwamba, balozi mdogo wa Syria Ihsan Raman aliwasili Riyadh na kutembelea Ubalozi wa Syria mjini humo.

Chanzo hicho, kikinukuu vyanzo vya kidiplomasia, pia kilieleza kuwa Damascus inapanga kumteua Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje, Ayman Sousan, kuwa balozi wake mdogo nchini Saudi Arabia, huku maandalizi ya ufunguzi rasmi wa Ubalozi wa Syria mjini Riyadh yakiendelea.

Raman aliteuliwa kuwa Balozi mdogo wa Syria nchini Saudi Arabia wakati wa mkutano wa wiki iliyopita wa Baraza la Syria. Hatua hii inalenga kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Syria na Saudi Arabia, ambao ulikatwa tangu 2011.

Mwezi Mei mwaka huu, Saudi Arabia na Syria zilitangaza uamuzi wa kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia, baada ya kupita zaidi ya muongo mmoja tangu Riyadh ilipochukua hatua ya kuvunja uhusiano huo na kuanza kuunga mkono makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakipambana na serikali ya Damascus.

Itakumbukwa kuwa Saudi Arabia na washirika wake walivunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Syria mwaka 2011 kufuatia kuzuka wimbi kubwa la machafuko na mapigano yaliyoanzishwa na makundi ya kigaidi yakichochewa na kuungwa mkono na muungano wa Magharibi na wa Waarabu dhidi ya taifa hilo la Kiarabu.