Saudi Arabia yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i102944-saudi_arabia_yalaani_kuvunjiwa_heshima_qur'ani_tukufu_nchini_sweden
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia imetoa taarifa maalumu na kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani huko nchini Sweden.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 01, 2023 23:02 UTC
  • Saudi Arabia yalaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia imetoa taarifa maalumu na kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima kitabu kitakatifu cha Qur'ani huko nchini Sweden.

Taarifa hiyo imesisitiza msimamo wa Saudi Arabia kuhusu kukataa kabisa vitendo hivi, ambavyo kwa bahati mbaya vimekuwa vikirudiwa kwa mpangilio katika miji mikuu kadhaa ya Ulaya kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza ili kuchochea hisia za mamilioni ya Waislamu duniani kote.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia imezitaka mamlaka za Sweden kushughulikia mara moja vitendo hivyo na kuacha kutoa leseni kwa kundi hilo lenye itikadi kali linalojihusisha na kuchochea chuki na ubaguzi wa rangi.

Salwan Momika jana alirudia tena kitendo kiovu na cha kishenzi cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu mjini Malmö kwa kibali rasmi cha Polisi ya nchi hiyo.

Katika miezi ya karibuni, Momika amechoma moto Msahafu mara kadhaa na kuibua hisia kali duniani za kukemewa, kupingwa na kulaaniwa kitendo chake hicho. Aliwahi kufanya kitendo hicho kiovu kwa kibali rasmi cha Polisi ya Sweden tena mbele msikiti mkuu wa Stockholm hata katika moja ya Sikukuu kubwa ya Waislamu ya Idul-Adhha iliyosadifiana na tarehe 28 Juni mwaka huu.

 

Mhamiaji huyo wa Kiiraq anayekabiliwa na kesi nyingine pia alirudia tena kitendo kiovu kwa kuchoma moto Msahafu mbele ya balozi za nchi za Kiislamu zikiwemo Iraq, Iran, Uturuki na Misri na kupelekea jumuiya za kikanda na kimataifa kutoa matamko ya kukemea na kulaani kitendo hicho.

Serikali na viongozi wa Sweden ambao wamedai mara kadhaa kuwa watachunguza vitendo hivyo kisheria na kisiasa wanaendelea kuunga mkono jinai hizo dhidi ya Uislamu na kuzidi kuchochea hisia za Waislamu duniani.