Hatua za kichochezi za Marekani kuunga mkono utawala wa Kizayuni
Kufuatia mashambulizi makubwa ya makundi ya mapambano na ukumbozi wa Palestina katika maeneo yanayouzunguka Ukanda wa Ghaza, ambayo yamedhihirisha udhaifu na utepetevu mkubwa wa utawala wa Kizayuni, Marekani imepanga na kutekeleza hatua za kichochezi kwa kisingizio cha eti kuiunga mkono Tel Aviv na kuimarisha ari ya Wazayuni.
Makundi ya muqawama ya Palestina yenye makao makuu yao katika Ukanda wa Ghaza, yaani harakati ya Hamas, pamoja na harakati nyingine za Palestina, hususan harakati ya Jihadul Islami, yalianzisha operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala wa Kizayuni siku ya Jumamosi, Oktoba 7, 2023, ambayo imeupelekea utawala huo kuchanganyikiwa na kuibua mshangao na mshtuko mkubwa miongozi mwa Wazayuni.
Kuhusiana na hilo Marekani inapanga kutuma manowari na ndege zake za kijeshi karibu na Palestina inayokaliwa kwa mabavu kama msaada kwa Tel Aviv. Lloyd Austin, Waziri wa Ulinzi wa Marekani alisema jana Jumapili kwamba ameamuru kuondoka manowari inayosheheni ndege za kivita ya Gerald Ford kuelekea mashariki mwa Mediterania ili kuimarisha juhudi za kuzuia mashambulio eti ya adui. Afisa mmoja wa Marekani pia ametangaza kuwa Marekani itapeleka ndege zake za kivita kati ya 20 hadi 25 aina ya F-15 na F-35 huko Asia Magharibi kama sehemu ya mpango wa kuimarisha nafasi ya vikosi vyake katika eneo hilo, ambazo baadaye zitatumwa katika Ghuba ya Uajemi. Mmarekani huyo amedai kuwa nadhumuni ya kutumwa ndege hizo za ziada za kivita ni kuimarisha hatua za kuzuia uwezekano wa mashambulio ya Iran au kupanua vita nje ya mipaka ya Israel.
Ni wazi kuwa hatua hizo za Washington zinalenga kuupa moyo utawala wa Kizayuni na kuwatia hofu waungaji mkono wa Wapalestina katika eneo hili. Hata hivyo, muqawama wa Wapalestina sio tu kwamba hautishwi na harakati hizo, bali umeionya Washington kuhusu tukio lolote la kichochezi katika eneo. Kuhusiana na hilo, msemaji wa Hamas amesema kuwa Marekani inapaswa kufahamu madhara ya kutuma manowari yake hiyo ya kubeba ndege za kivita karibu na Israel. Msemaji huyo wa Hamas amesisitiza hilo kwa kusema: "Tangazo la Marekani la kupeleka manowari ya kubeba ndege za kivita katika eneo kwa ajili ya kuisaidia Israel ni kushiriki moja kwa moja katika uchokozi dhidi ya watu wetu."
Licha ya hitilafu za kimbinu zilizopo kati ya Rais Joe Biden wa Marekani na Binjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Marekani ikiwa ni muungaji mkono mkuu asiye na masharti wa Israel, daima imekuwa ikivitaja vitendo vya jinai vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kuwaua kigaidi, kuwa ni hatua ya kujilinda utawala huo wa kibaguzi. Imekuwa ikiunga mkono wazi wazi hatua za utawala huo za kuendelea kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuupa misaada mikubwa zaidi ya kijeshi na kifedha kati ya nchi zote za Magharibi, ili kuuwezesha kuendelea kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya watu hao wasio na hatia wala ulinzi. Kuhusiana na hilo, baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, serikali ya Biden imetangaza kuwa itatuma haraka zana za ziada za kijeshi kwa jeshi la Kizayuni.
Kabla ya hapo, Anthony Blinken Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani sambamba na kuashiria dhamira ya Biden ya kuendelea kudhamini usalama wa utawala wa Kizayuni amesema: "Tutahakikisha kuwa Israel inapata zana inazohitaji kujilinda." Uhusiano wa kimkakati wa Marekani na Israel siku zote umekuwa ukiungwa mkono na marais wote wa Marekani. Hususan kuzidi kuuimarisha kijeshi utawala wa Kizayuni na kuupa uungaji mkono wa pande zote katika ukandamizaji na mauaji ya Wapalestina kwa kisingizio cha kujilinda, ni siasa zinazopewa kipaumbele na Washington kuhusiana na Israel.
La muhimu ni kwamba, serikali ya Biden imekuwa na matumaini makubwa ya kufikiwa haraka mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni, lakini hivi sasa juhudi hizo zote zimesambaratishwa na operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Gazeti la Marekani la New York Times limeandika kuwa, mashambulizi ya Hamas dhidi ya Tel Aviv yameondoa matumaini ya Rais Joe Biden wa Marekani ya kufanya mazungumzo na kuleta mshikamano mkubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati kupitia kuanzishwa uhusiano kati ya Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni. Washington, ambayo hadi sasa ilikuwa imeliweka pembeni suala la Palestina, hasa kuhusu suluhisho la kubuniwa nchi mbili, kufuatia mazungumzo ya kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida kati ya Riyadh na Tel Aviv, hivi sasa imelegeza msimamo wazi wazi, na kuchukua msimamo tofauti.
Kuhusiana na suala hilo, Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema Jumapili kwamba njia bora ya kutatua tatizo kati ya utawala wa Kizayuni na Wapalestina ni suluhisho la nchi mbili. Licha ya misimamo hiyo, lakini muqawama wa Wapalestina kupitia operesheni yake ya kihistoria na isiyo na mfano wake ya hivi karibuni, umethibitisha kivitendo kuwa, njia zinazodaiwa kuwa ni za suluhu ya amani na Israel hazina tija yoyote na kwamba haki za Wapalestina zitapatikana tu kupitia mapambano na kuutwisha utawala huo ghasibu matakwa yao.