Hamas yajibu matamshi ya kichochezi ya Biden juu ya Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekosoa vikali matamshi yaliyotolewa na Rais Joe Biden wa Marekani na kusisitiza kuwa, matamshi hayo ya kichochezi yanalenga kukoleza moto wa jinai za utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Hamas imesema kauli ya Biden kuhusu harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu na wakazi wa Ukanda wa Gaza ni ya upotoshaji na inakusudia kuficha jinai na mienendo ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni.
Taarifa ya Hamas imesema, "Sisi ndani ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina tunapinga na kulaani matamshi ya kichochezi ya Rais Joe Biden wa Marekani; matamshi yanayolenga kuuchochea utawala wa Kizayuni ushadidishe taharuki mkabala wa Wapalestina."
Hamas imesema matamshi hayo yaliyotolewa na Biden siku ya Jumanne yamejaa makosa ya kisiasa na kisheria, na yameegea upande wa utawala katili, wa kibaguzi na unaochukiwa zaidi katika eneo la Asia Magharibi.
Biden juzi Jumanne, sambamba na kulaani Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, alidai kuwa Hamas haitetei wala kupigania haki za taifa la Palestina. Aliendelea kubwabwaja kwa kusema: Azma ya Hamas ni kuisabaratisha Israel na kuwaua Mayahudi.
Kadhalika alifananisha vitendo vya Hamas na vya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS). Hii ni katika hali ambayo, Hamas inasisitiza kuwa, wanamapambano wa Palestina na wapiganaji wa tawi lake la kijeshi, Brigedi za al-Qassam, wanaepuka raia, na wanalenga tu mfumo wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Operesheni Kimbunga cha al-Aqsa.
Hamas imekanusha madai yanayotolewa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kwamba wapiganaji wake wanalenga watoto, ikitoa wito kwa vyombo hivyo vya habari kuwa makini na kutoegemea upande wa Wazayuni.