Haniyeh: Marekani inabeba dhima ya jinai ya hospitali ya al-Maamadani
Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Masuala ya Kisiasa ya Hamas, ameyachukulia mauaji ya hospitali ya al-Maamadani kuwa kielelezo cha kushindwa kwa fedheha kwa adui Mzayuni na akasema kwamba Wamarekani ambao wanatoa uungaji mkono usio na kikomo kwa adui huyo wanahusika moja kwa moja na jinai ya hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA; Haniyeh amebainisha kuwa jinai hiyo ya kinyama ya adui inaonyesha ukatili wake ambao amekuwa ukiutenda dhidi ya Wapalestina tokea akalie kwa mabavu ardhi zao.
Akieleza kuwa adui Mzayuni haheshimu maadili, sheria wala kanuni zozote, ameendelea kusema: Waliofanya jinai ya Hospitali ya Maamadani ni wale wale waliowaua kigaidi wakazi wa Sabra na Shatila, wakatenda jinai ya shule ya Bahr al-Baqr pamoja na kuwaua mateka wa jeshi la Misri.
Haniyeh amesema kuwa Adui amekosea kabisa ikiwa anadhani kwamba kwa mauaji hayo anaficha kushindwa kwake kwa fedheha au kulisalimisha taifa la Palestina. Ameongeza: Mapambano yanaendelea na yatasimam pale tu wavamizi watakapoondoka kwenye ardhi na maeneo matukufu ya Wapalestina.
Wavamizi hao wa Kizayuni wameishambulia kwa mabomu hospitali ya al-Maamadani huko Gaza jana Jumanne na kupelekea Wapalestina 500 kuuawa shahidi katika tukio hilo.
Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas ametangaza siku tatu za maombolezo ya taifa kufuatia mauaji ya halaiki katika hospitali ya al-Maamadani katika Ukanda wa Ghaza. Kufuatia jinai za kivita na mashambulizi ya kinyama ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika hospitali za Ghaza na mauaji ya kimbari ya mamia ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia imelaani jinai hiyo na kutangaza Jumatano ya leo kuwa siku ya maombolezo ya kitaifa kote nchini.