Madola ya Magharibi yalaumiwa kwa unafiki kuhusu vita vya Gaza
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeyatuhumu madola ya Magharibi kwa kile ilichosema kuwa unafiki na undumakuwili kwa kushindwa kukemea jinai zinazofanywa na utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Naibu Mkurugenzi wa Programu katika shirika hilo la kimataifa, Tom Porteous, amesema kuwa, tangu Oktoba 7 yalipofanyika mashambulizi ya Harakati ya Hamas dhidi ya Israel, ni kama kauli za Marekani na Ulaya zimenyamazishwa huku akihoji ni kwa nini vitendo vya kuizingira Gaza kwa miaka 16, ambavyo amesema ni sawa na adhabu ya jumla na uhalifu wa kivita, havikemewi.
Afisa huyo wa Human Rights Watch amesema kuheshimiwa sheria ya kimataifa juu ya haki za binaadamu inayodhamiria kuwalinda raia ni jambo linalowahusu watu wote duniani huku akihoji pia juu ya kukosekana wito ulio wazi kama ilivyokuwa katika mzozo wa Ukraine, wa kuitaka Israel iheshimu kanuni za kimataifa katika mashambulizi yake dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Hii si mara ya kwanza kwa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani kuwa na unafiki katika masuala mbalimbali hasa ya haki za binadamu ambapo kama ilivyo katika vita vya Ukraine unafiki wao umeshudiwa kwa mara nyingine katika vita vya Gaza na hasa mashambulio na jiinai za Israel dhidi ya raia wasio na hatia.
Hata shambulio la kinyama la utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Hospitali ya al-Ma'madani limenyamaziwa kimya na Marekani na washirika wake ambapo mamia ya watu wameuawa kinyama.
Hii leo wale wanaodai kutetea haki za binadamu na ambao wanatekeleza malengo yao ya kisiasa kwa kutumia mashinikizo wameifumbia macho kabisa Gaza na dhulma inayofanywa dhidi ya wananchi wa Palestina.