Mpasuko waripotiwa katika baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel
Gazeti la Israel la Yedioth Ahronoth limeripoti kuwa, kuna mgogoro wa kutoaminiana kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na uongozi wa jeshi lake, na kwamba uhusiano wake na Waziri wa Ulinzi katika serikali yake, Yoav Galant, unayumbayumba, jambo ambalo linazuia ushirikiano wa kikazi baina ya wawili hao.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti hilo imeonyesha kuwa, mawaziri wasiopungua watatu katika serikali ya dharura ya Israel wanafikiria kujiuzulu ili kumlazimisha Netanyahu kuwajibika kwa kushindwa kiusalama baada ya operesheni ya Hamas ya Kimbunga cha al Aqsa.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa, asilimia 75 ya Waisraeli wanambebesha Netanyahu dhima ya kushindwa kulinda miji na vitongoji vya kandokando ya Ukanda wa Gaza ambavyo vilishambuliwa na wanamapambano wa Wapalestina wakati wa Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Gazeti hilo limesema kuwa kuna hitilafu kati ya Netanyahu na maafisa wakuu wa jeshi kuhusiana na tathmini, mipango na maamuzi ya masuala mbalimbali.
Gazeti la Yedioth Ahronoth limenukuu vyanzo vya kisiasa na kijeshi vya Israel na kusema kwamba, Netanyahu amewakasirikia maafisa wakuu katika jeshi na anapokea kwa tahadhari kubwa maoni na tathmini zinazotolewa na viongozi wa jeshi, na kwamba uhusiano mbaya kati yake na Waziri wa Ulinzi, Galant unatatiza zaidi ushirikiano baina ya pande hizo mbili.
Itakumbukwa pia kwamba serikali yenye misimamo ya kupindukia mipaka ya Waziri Mkuu katili wa Israel, Benjamin Netanyahu, inakabiliwa na malalamiko makubwa na maandamo ya miezi kadhaa sasa ya wanaomtaka ajiuzulu na halafu apandishwe kizimbani kwa tuhuma za ufisadi wake yeye, na familia yake.
Sababu kuu iliyozidisha mashinikizo ya kutaka Netanyahu ajiuzulu, ni mpango wake wa kufanyia marekebisho mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni ili kuivunja nguvu idara ya mahakama na kuizidishia nguvu serikali. Wapinzani wa Netanyahu wanasema kuwa mpango huo ni sehemu ya njama za Waziri Mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni za kutawala kidikteta na kuidhibiti mihimili mengine ya dola ili awe salama mbele ya shutuma nzito za ufisadi zinazomkabili.