Erdogan: HAMAS si kundi la magaidi, bali wapigania ukombozi
(last modified Thu, 26 Oct 2023 12:23:34 GMT )
Oct 26, 2023 12:23 UTC
  • Erdogan: HAMAS si kundi la magaidi, bali wapigania ukombozi

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amefuta safari yake ya kuzitembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kupachikwa jina bandia la Israel na kusisitiza kuwa, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS si kundi la magaidi, bali ni kundi la wapigania ukombozi.

Erdogan ameukosoa vikali utawala wa Kizayuni kwa kutumia vibaya 'nia njema' ya Uturuki na kueleza kuwa, "Uhusiano (wetu na Israel) ungekuwa tofauti, lakini kwa masikitiko hilo halitafanyika tena."

Amelaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kubainisha kuwa, asilimia 50 ya waliouawa shahidi katika eneo hilo ambalo liko chini ya mzingiro ni watoto wadogo.

Rais wa Uturuki alisema hayo jana katika hotuba yake mbele ya mkutano wa wabunge wa chama tawala cha AK mjini Ankara na kueleza bayana kuwa: HAMAS si mtandao wa kigaidi, bali ni kundi la wapigania ukombozi na mujahidina wanaopambana kulinda ardhi na taifa lao.

Kadhalika amewatuhumu wa Wamagharibi kwa unafiki na undumakuwili kwa kufeli kuzuia mauaji ya halaiki ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Israel kwa makusudi katika Ukanda wa Gaza. 

Mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza

Aidha Rais Erdogan ametoa mwito kwa mataifa ya Waislamu kushirikiana na kuwa kitu kimoja katika kukomesha jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.

Kadhalika Rais wa Uturuki mapema leo Alkhamisi amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis na kubainisha kuwa: Mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ni mauaji ya kimbari, na kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa jinai hizo ni fedheha kwa jamii ya wanadamu.

 

Tags