Kupungua kwa kasi umaarufu wa Netanyahu katika chama chake
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yanaonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa umaarufu wa Benjamin Netanyahu miongoni mwa wakaazi wa ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, matokeo ya uchunguzi mpya wa gazeti la Kizayuni la "Ma'ariv" yanaonesha kuwa, ni asilimia 27 tu ya wakaazi wa maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu wanaomkubali Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kama mgombea anayefaa wa nafasi hiyo. Kwa upande mwingine, asilimia 49 ya wakazi wa maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu wanaamini kwamba, Benny Gantz, kiongozi wa muungano wa upinzani wa Blue and White ni chaguo bora kuliko Netanyahu katika nafasi ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni. Uchunguzi huo wa maoni umefanyika kwa kuwashirikisha wakazi 522 wa ardhi zilizonyakuliwa na kukaliwa kwa mabavu na maghasibu wa Kizayuni.
Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa umaarufu wa chama tawala cha Likud kinachoongozwa na Benjamin Netanyahu umeshuka kwa kiasi kikubwa kufuatia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza na kushindwa utawala huo kukabiliana na operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa.
Tarehe 7 Oktoba Hamas ilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na utawala wa Kizayuni kutokea Ukanda wa Ghaza. Katika kulipiza kisasi cha operesheni hiyo iliyotekelezwa katika kukabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na vile vile kuvunjiwa heshima Msikiti wa Al-Aqsa, Tel Aviv ilianza mauaji ya kimbari dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina na kuzuia kufikishwa chakula, dawa, mafuta na huduma nyingine muhimu za maisha kwa wakazi wa Ghaza.
Mashambulizi ya ghafla ya wanamapambano wa Palestina kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yamepelekea kupungua sana umaarufu na uungaji mkono kwa Benjamin Netanyahu na baraza lake la mawaziri miongoni mwa Wazayuni hao.