Afrika Kusini: Vitendo vya Israel Gaza ni jinai za kivita
-
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
Rais wa Afrika Kusini amesema kuwa vitendo vya utawala wa Kizayuni Ukanda wa Gaza ni jinai za kivita.
Shirika la habari la Irna limeripoti kuwa, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye ameelekea nchini Qatar kwa ziara rasmi amesema katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza kwamba: Vitendo vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni jinai za kivita.
Rais wa Afrika Kusini amedhihirisha msimamo huu katika hali ambayo Jumamosi tarehe 11 ya mwezi huu wa Novemba pia makumi ya maelfu ya wakazi wa mji wa Cape Town nchini Afrika Kusini walifanya maandamano ya kuiungamkono Palestina na kulaani jinai za Israel khususan maangamizi ya kizazi na mauaji ya watoto yanayofanywa na utawala huo huko Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti hii, wafanya maandamano walitaka kusitishwa vita haraka iwezekanavyo, kutolewa misaada ya kibinadamu kwa raia wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza, kuhukumiwa viongozi wa utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na kukombolewa Palestina.
Waandamanaji huko Afrika Kusini walitaka pia kufukuzwa nchini humo Balozi wa utawala wa Kizayuni. Maandamano haya tajwa ambayo ni miongoni mwa mikusanyiko isiyo na kifani kuwahi kushuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni huko Afrika Kusini kwa kuzingatia idadi ya washiriki, yalifanyika kufuatia mwaliko wa vyama zaidi ya 40 vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kidini za Waislamu, Wakristo na Wayahudi.