OIC yakosoa ripoti ya US, EU na UN kuhusu Palestina
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imekosoa ripoti ya pande nne za Marekani, Russia, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kuhusu mgogoro wa Palestina na utawala haramu wa Israel na kusisitiza kuwa, ripoti hiyo imeegemea upande wa kuiunga mkono Tel Aviv.
Iyad bin Amin Madani, Katibu Mkuu wa OIC ameitaja ripoti hiyo ya kurasa 8 ya Marekani, Russia, UN na EU kuwa imejaa makosa, haina msingi wala malengo na mapendekezo yake ni kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel.
Madani amekosoa vikali ripoti hiyo iliyosema kuwa, kubuniwa mataifa mawili ndiyo njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Israel na Palestina pasina kuupa kipaumbele ufumbuzi wa kisiasa. Ripoti hiyo iliyotolewa Ijumaa iliyopita imesema, hiyo ndiyo njia pekee ya kupatikana amani ya kudumu katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imelitaka kundi hilo la pande nne kuwa mpatanishi asiyeegemea upande wowote. OIC imelitaka kundi hilo kuandaa ramani ya njia ya kuhakikisha kuwa nchi huru ya Palestina linaundwa sawa na kusimamisha ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.