Matokeo ya kiuchumi ya vita vya Gaza kwa utawala wa Kizayuni
(last modified Sun, 19 Nov 2023 11:24:01 GMT )
Nov 19, 2023 11:24 UTC
  • Matokeo ya kiuchumi ya vita vya Gaza kwa utawala wa Kizayuni

Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya tarehe 7 Oktoba ambayo imeupelekea utawala haramu wa Israel kupata kipigo kikubwa kihistoria imeupelekea pia utawala huo kuendelea kushindwa katika nyanja nyingine hasa ikitiliwa maanani kwamba ungali unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa imeusababishia utawala huo wa Kizayuni hasara kubwa ya kifedha isiyo na mfano wake. Hasara hiyo inaweza kuchunguzwa katika sehemu mbili, ya  moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja. Hasara za moja kwa moja zinatokana na gharama za vita hivyo na zisizokuwa za moja kwa moja ni za mabilioni ya dola yanazopata mashirika na makampuni pamoja na miundombinu ya utawala wa Kizayuni kutokana na taathira za vita hivyo.

Kanali ya Telegramu ya tovuti ya Kipalestina ya Al-Risalah imetoa ripoti na kuashiria takwimu za hasara za kiuchumi za karibu dola bilioni 100 za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja ulizopata utawala ghasibu wa Kizayuni tokea mwanzo wa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa hadi siku za 17 za vita hivyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, thamani ya shekeli (sarafu ya utawala wa Kizayuni) ilipungua kwa asilimia 5.7. Uharibifu wa moja kwa moja kwa miundombinu ulikuwa wa dola bilioni 4 na wa sekta ya utalii dola bilioni 3.5. Kupungua kwa asilimia 10 ya miamala ya soko la hisa la Tel Aviv, yaani, thamani ya dola bilioni 29 ni jambo ambalo limeutia utawala huo wasi wasi mkubwa. Kusimamishwa uzalishaji wa gesi pia kulikuwa kumeacha nyuma hasara ya dola bilioni 6. Kusimamishwa shughuli katika bandari ya Ashkelon kulisababisha hasara ya dola bilioni 24. Hundi za hisa zilipungua kwa asilimia 10. Gharama ya moja kwa moja ya operesheni za kijeshi ilikuwa imefikia dola bilioni 7.

Askari wa Kizayuni huko Gaza

Aidha utawala wa Kizayuni umewarejesha jeshini askari wa akiba wapatao 360,000 kati ya askari 400,000 kwa ajili ya vita hivyo vinavyoendelea kuugharimu utawala huo pesa nyingi. Kwa upande mwingine, kuondolewa kiasi kikubwa cha wafanyakazi katika viwanda na vituo vya taaluma na kielimu kumeleta madhara mengine yasiyo ya moja kwa moja kwa uchumi wa utawala huo. Karibu asilimia 8 ya wafanyakazi wameitwa kutoa huduma za dharura za kijeshi, suala ambalo limepelekea utawala huo wa kibaguzi kukabiliwa na uhaba mkubwa wa wafanyakazi viwandani. Kulingana na ripoti zilizopo, bandari ya Haifa pia inakaribia kufungwa na hakuna meli za kigeni zinazotia nanga hapo.

Mbali na hayo utawala wa Kizayuni umewahamisha walowezi wapatao 250,000 kutoka vitongoji vya walowezi kaskazini mwa mpaka na Lebanon na kuwapeleka kusini mwa Eilat. Pia imehamisha walowezi wa Kizayuni katika vitongoji 55 karibu na mpaja wa Ukanda wa Gaza ambavyo vina wakaazi wapatao 50,000. Hata hivyo, Wazayuni wasiopungua laki tatu ndani ya utawala wa Kizayuni wamehamishwa kutoka makwao na kupelekwa katika maeneo mengine, jambo ambalo limeugharimu utawala huo mabilioni ya dola. Wakati huo huo, kukimbia walowezi wa Kizayuni kutoka maeneo ambayo wamekuwa wakiishi kumevuruga shughuli za kawaida za biashara na kupelekea kufungwa maduka mengi, vituo vya matibabu, shule, huduma za usafiri katika maeneo ambayo yanashambuliwa kwa maroketi ya Hamas.

Suala jingine ni kwamba, vita vya Gaza vimepelekea kusimama uwekezaji wa kigeni na vilevile wa ndani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa sababu uwekezaji unahitaji utulivu na usalama, mambo mawili ambayo hayako tena kutokana na vita vinavyoendelea.

Ni kutokana na matokeo hayo ya kiuchumi ndio maana wengi wanaamini kuwa, kuendelea vita si tu kwamba hakutauletea utawala wa Kizayuni ushindi wowote, bali pia kutauongezea matatizo zaidi ya kijeshi, kiuchumi na kisiasa.