Israel yashambulia makao makuu ya Hilali Nyekundu Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i106466-israel_yashambulia_makao_makuu_ya_hilali_nyekundu_gaza
Vikosi vya jeshi katili la utawala haramu wa Israel vimeshambulia kwa mabomu makao makuu ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-12-26T23:23:47+00:00 )
Dec 26, 2023 23:23 UTC
  • Israel yashambulia makao makuu ya Hilali Nyekundu Gaza

Vikosi vya jeshi katili la utawala haramu wa Israel vimeshambulia kwa mabomu makao makuu ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Mashambulizi hayo ya kinyama yameharibu sehemu kubwa ya majengo ya taasisi hiyo ambayo yalikuwa yanawahifadhali maelfu ya wakimbizi wa ndani katika eneo hilo lililozingirwa.

Kanali ya Press TV imemnukuu Msemaji wa Hilali Nyakundu ya Palestina akisema kuwa, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni jana Jumanne zilishambulia eneo hilo huko magharibi mwa mji wa Khan Younis na kusababisha uharibifu mkubwa.

Amesema hivi sasa hakuna eneo lolote ambalo ni salama kwa Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, huku utawala wa Kizayuni ukishadidisha mashambulizi yake ya angani na ardhini katika ukanda huo.

Jinai za Wazayuni Gaza

Jana Jumanne, jeshi la Israel kwa majivuno lilisema kuwa ndege za kijeshi za utawala huo zimeshambulia maeneo zaidi ya 100 kusini mwa Ukanda wa Gaza ndani ya saa 24.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, watu zaidi ya 241 waliuawa shahidi huku wengine 382 wakijeruhiwa katika kipindi cha saa 24 hapo jana, kutokana na hujuma za kutisha za utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Wapalestina karibu 21,000 wameshauawa shahidi tokea Oktoba 7 hadi sasa kutokana na mashambulio hayo ya kinyama ya jeshi la Kizayuni huko Gaza, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.