Himaya mpya ya Magharibi kwa Israel
Wakati ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel bado unaendeleza mauaji yake dhidi ya Wapalestina wa Gaza, nchi za Magharibi nazo zinaendelea kutoa himaya na misaada kwa utawala huo, na kinyume na madai yote ya eti kutetea haki za kibinadamu yanayotolewa na nchi hizo, zinaiwezesha Israel kuendeleza vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.
Kuhusiana na jambo hilo serikali ya Ujerumani imetangaza kuwa imepata kibali cha awali kutoka idara husika za Wizara za Mambo ya Nje na Ulinzi za nchi hiyo cha kutuma silaha na mizinga kwa utawala haramu wa Israel.
Gazeti la Der Spiegel limenukuu duru za habari na kusema: Berlin inachunguza suala la kutuma risasi za vifaru na mizinga zinazohitajiwa na jeshi la Israel ili kuendeleza vita katika Ukanda wa Gaza na kuiunga mkono Tel Aviv katika medani zote za kikanda.
Utoaji leseni za kusafirisha zana za kijeshi za Ujerumani kwenda Israel umeongezeka mara 10 katika miezi ya hivi karibuni sambamba na kustadi mashambulizi ya utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina ikilinganishwa na hapo awali, na Berlin inatoa kipaumbele sana kwa suala hilo.
Ujerumani inalipa umuhimu suala la kuiuzia silaha Israel, huku makumi ya Wapalestina wakiuawa shahidi na kujeruhiwa kila siku katika mashambulizi ya utawala huo ghasibu. Idadi ya mashahidi wa Kipalestina huko Gaza katika siku mia moja ya mashambulizi hayo imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 24,000. Hii ni katika hali ambayo Gaza inakabiliwa na mgogoro mkubwa. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, asilimia 15 ya wakazi wa Gaza wako katika hali ya maafa na wanasumbuliwa na njaa, na kwamba Wapalestina zaidi ya milioni moja waliolazimika kuwa wakimbizi wanaishi katika mazingira magumu.
Katika hali hiyo na wakati nchi nyingi za dunia zinalaani unyama na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Gaza, sambamba na kufanya jitihada za kukomesha mashambulizi, na kurejesha amani na kuanda uwanja wa kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa Gaza, nchi za Magharibi, ikiwemo Ujerumani, zinaendelea kuiunga mkono waziwazi Israel na kuruhusu kutumwa silaha na zana za kijeshi za kuendeleza maangamizi ya kizazi cha Wapalestina wa Gaza.
Hii ni pamoja na kuwa, nchi hizo za Magharibi pia zimeanza kutoa mashinikizo kwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inayoshughulikia mashtaka ya mauaji ya kimbari yaliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel. Kesi ya jinai za Israel dhidi ya watu wa Gaza ilianza kusikilizwa rasmi wiki iliyopita katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, na nchi nyingi za dunia zimeunga mkono mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya Israel. Suala hilo limezifanya nchi za Magharibi kuipatia Israel silaha zaidi, na kuzidisha uungaji mkono wao wa kisiasa kwa utawala huo. Kwa kadiri kwamba, serikali ya Ujerumani ilitangaza uungaji mkono wake kwa Tel Aviv baada tu ya kikao cha kwanza cha kusikiliza kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala huo haramu katika mahakama ya ICJ.
Dmitry Polyansky, Naibu Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, anasema: "Vita vya Gaza vimeanika na kuiweka wazi siasa za kindumakwili za nchi za Magharibi, na hazithubutu hata kutaja vitendo viovu vya Israeli kama vilivyo."
Serikali ya Ujerumani ilipinga rasmi mashtaka ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala wa Kizayuni huko Gaza na kutangaza kuwa, iko tayari kushiriki katika vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ikiwa ni upande wa tatu ili kufafanua vipengee vya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1948.
Kulaaniwa jinai za utawala ghasibu wa Israel katika jumuiya za kimataifa na kushindwa Tel Aviv kutetea jinai zake dhidi ya Wapalestina katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kumezidisha himaya ya nchi za Magharibi kwa utawala huo katili. Katika mkondo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amekutana na Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Tariq Ahmad Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amesema: Tumefanya kikao cha pamoja na David Cameron Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza na vilevile Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.
Nchi za Magharibi hususan Ujerumani na Uingereza zinajaribu kuathiri maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na vikao vya kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni kwa kushauriana na kutoa mashinikizo dhidi ya mahakama hiyo.
Bila kujali kauli mbiu zao zote za kibinadamu, nchi za Magharibi, kwa upande mmoja, zinadai kutetea haki za kibinadamu, na kwa upande mwingine, zinaiimarisha Israel na kutetea misimamo ya Tel Aviv. Kwa muktadha huo nchi hizo ni wanashirika katika jinai za Israel dhidi ya watu wa Wapalestina.