Jun 16, 2024 02:44 UTC
  • Hizbullah yayatwanga tena kwa makombora maeneo ya Wazayuni

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imefanya mashambulio mapya dhidi ya maeneo ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuuni ikiwa ni kujibu mauaji ya hivi karibuni ya Israel ya kamanda mmoja mkubwa wa harakati hiyo huko kusini mwa Lebanon.

Sami Abdallah, anayejulikana zaidi kwa jina la Abu Talib, aliuawa shahidi pamoja na watu wengine watatu katika mashambulizi ya Israel ambayo yalilenga jengo la makazi ya watu katika mji wa Jwaya wa kusini mwa Lebanon Jumanne iliyopita.

Hizbullah ilisema katika taarifa tofauti jana Jumamosi kwamba vikosi vyake vimepiga kwa makombora ya kuongozwa kwa mbali, vifaa vya kijasusi vya Israel na mifumo ya rada kwenye Mlima Meron pamoja na kundi la askari wa utawala huo ghasibu ikiwa pia ni katika kuendelea kuwaunga mkono Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.

Sehemu moja ya taarifa ya Hizbullah imesema: "Katika kuunga mkono watu wetu imara wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza na kuunga mkono muqawama wao wa kijasiri na wa heshima, na ikiwa pia ni sehemu ya jibu la mauaji yaliyofanywa na adui Mzayuni katika mji wa Jwaya, wanamuqawama wa Kiislamu, wamepiga makao makuu ya Kitengo cha Ufuatiliaji na Uendeshaji wa Anga katika kituo cha Meron cha Wazayuni kwa makombora ya kuongozwa kwa mbali sambamba na kuteketeza sehemu ya vifaa na rada zake.

Vile vile Hizbullah imesema: Imelipiga kwa makombora kundi la askari wa adui Mzayuni na kusababisha kungamia baadhi yao na wengine kujeruhiwa.

Tags