Umoja wa Mataifa: Vita vimeigeuza Gaza kuwa Jahanamu ya duniani
(last modified Tue, 18 Jun 2024 02:43:48 GMT )
Jun 18, 2024 02:43 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Vita vimeigeuza Gaza kuwa Jahanamu ya duniani

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vita vimeligeuza eneo la Ukanda wa Gaza kuwa Jahanamu ya duniani.

Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu ametangaza kuwa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Ukanda wa yameligeuza eneo hilo linalokabiliwa na changamoto nyingi kama umasikini na ukosefu wa huduma muhimu kuwa Jahanamu ya duniani.

Aidha amesema, takribani imekuwa ni muhali kupeleka misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza ambao wako kwenye hatihati ya njaa.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema pia kuwa, viongozi wa dunia wametuangusha na baadhi yao wanaendelea kuuunga mkono bila masharti utawala wa Kizayuni licha ya kuwepo nyaraka na ushahidi wa ukiukwaji wa sheria na haki binadamu unaofanywa na utawala huo.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu amebainisha kuwa, licha ya madhara ya kutisha ya vita dhidi ya raia wa Gaza, lakini usafirishaji wa silaha kutoka Marekani na nchi nyingine hadi Tel Aviv unaendelea kushuhudiwa.

Hivi karibuni Kamati ya kutafuta ukweli ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa, utawala unaokalia kwa mabavu wa Quds umefanya "maangamizi" ya Wapalestina wakati wa vita dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Miezi minane ikiwa imepita tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya kikatili dhidi ya Gaza, sehemu kubwa ya majengo ya eneo hilo yamegeuka magofu huku jeshi la Kizayuni likiendelea kuweka kizuizi cha kufikishwa chakula, maji safi na dawa kwa wakazi wa eneo hilo wanaoatilika kwa njaa.

 

Tags