Yemen: Tuko tayari kwa vita vya muda mrefu na Israel, ni baada ya Israel kushambulia al-Hudaydah
-
Brigedia Jenerali Yahya Saree
Vikosi vya Jeshi la Yemen vimeapa kuendeleza operesheni zinazoiunga mkono Palestina baada ya utawala haramu wa Israel kushambulia maeneo ya raia katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree aliyasema hayo jana Jumamosi, saa chache baada ya ndege za kivita za Israel kushambulia majengo, vituo vya mafuta na kituo cha umeme katika mkoa wa al-Hudaydah, magharibi mwa Yemen na kuua watu kadhaa.
Brigedia Jenerali Saree ameyataja mashambulizi hayo ya anga kuwa ni "uchokozi mbaya" ambao umelenga miundo mbinu ya kiraia.

Afisa huyo ameongeza kuwa, vikosi vya Jeshi la Yemen "havitasimamisha operesheni za kuwatetea ndugu zetu huko Gaza, bila kujali matokeo na athari zake."
Jeshi la Yemen limekuwa likishambulia ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) pamoja na meli za Israel au meli zenye mfungamano na utawala huo ghasibu tangu tarehe 7 Oktoba, wakati Tel Aviv ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Saree amesisitiza kwamba, vikosi vya jeshi la Yemen "vimejiandaa kwa vita vya muda mrefu na adui huyu hadi uchokozi dhidi ya Gaza utakapokoma, mzingiro uondolewe, na uhalifu wote unaofanywa dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza ukomeshwe."
Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema: "Vikosi vya Jeshi la Yemen vitajibu uchokozi huu mbaya na havitasita kulenga shabaha muhimu za adui, Israel."