UN: Utapiamlo unatishia maisha ya wajawazito na vichanga Gaza
Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNPF) umetahadharisha kuhusu taathira hasi za utapiamlo zinazowakodolea macho wanawake wajawazito na watoto wachanga katika Ukanda wa Gaza; huku vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina katika eneo hilo vikishadidi.
Taarifa ya UNFP iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X kwa lugha ya Kiarabu imeeleza kuwa, "Utapiamlo huko Gaza ni hatari kubwa kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga, huku kukiwa na ongezeko la kesi za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, wenye uzito wa chini na walioko katika hatari ya kuchelewa kukua."
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kufuatilia idadi ya watu duniani limebainisha kuwa: Imezidi kuwa jambo la kawaida kwa watoto kuzaliwa wakiwa na uzito wa chini huko Gaza. Watoto wengi hawakui ipasavyo kutokana na utapiamlo unaowapata wajawazito na vitoto vichanga.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Dunia (WHO) limetahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, watoto zaidi ya 8,000 wenye chini ya miaka 5 huko Gaza wanasumbuliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu kutokana na vita vya kikatili na vya mauaji ya kimbari vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel.

Aidha wiki iliyopita pia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) lilionya kuwa, takriban watoto 3,000 wa Kipalestina wapo katika ncha ya kuaga dunia mbele ya macho ya jamaa zao kwa kukosa matibabu ya utapiamlo wa kiwango cha juu kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Haya yanaripotiwa huku Ofisi ya Upashaji Habari ya Serikali huko Gaza ikiripoti hapo awali kuwa, watoto 34 walipoteza maisha kwa njaa hivi karibuni katika eneo hilo, huku wengine 3,500 wakiwa katika hatari ya kuaga dunia kutokana na utapiamlo na njaa.