Jul 31, 2024 09:21 UTC
  • Makundi mbalimbali yalaani mauaji ya Israel dhidi ya Ismail Haniyeh

Makundi ya mapambano na Muqawama, yamelaani kitendo cha kigaidi cha kuuawa Ismail Haniyeh, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) kufuatia shambulio dhidi ya sehemu alikofikia mjini Tehran.

Katika taarifa yake, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetuma salamu za rambirambi kwa taifa kubwa la Palestina, Umma wa Kiislamu na wa Kiarabu na watu wote huru duniani kutokana na kuuawa shahidi Ismail Haniyeh na kuongeza kuwa, Haniyeh ameuawa shahidi na Wazayuni akiwa mjini Tehran. 

Taarifa ya Hamas imesema, Ismail Haniyeh aliuawa shahidi kutokana na mashambulizi ya kihaini ya Wazayuni kwenye makazi yake mjini Tehran.

Moussa Abu Marzouq, mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, amesema kwamba, mauaji hayo hayatapita hivi hivi bila jibu.

Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen imetangaza katika taarifa yake kwamba, mauaji ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas mjini Tehran ni jinai ya kigaidi na ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Harakati ya Jihad ya Kiislami ya Palestina pia sambamba na kutuma salamu za rambirambi kutokana na mauaji ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, imesisitiza udharura wa kuendelezwa mapambano ya ukombozi wa Palestina na Muqawama dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Naibu katibu Mkuu wa Jihad Islami ya Paletina, Muhammad al Hindi amesema, kama adui anadhani kwamba anaweza kushinda mapambano na kuzima Muqawama kwa kuwaua viongozi wake, amefanya kosa kubwa.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas, amelaani mauaji ya Haniyeh na kuyataja kuwa ni "kitendo cha woga na tukio hatari."

Taarifa iliyotolewa na Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imesema: Jinai hii itaimarisha zaidi mshikamana baina ya wanamapambano dhidi ya adui wa pamoja.

Maulana Fazal ur Rehman, kiongozi wa Jamiat Ulema-e-Islam nchini Pakistan ametoa salamu za rambirambi kwa Ulimwengu wa Kiislamu na taifa la Palestina kwa mauaji ya kidhalimu ya mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas na kusisitiza kuwa, harakati za ukombozi wa Palestina na Quds Tukufu na vita dhidi ya adui Mzayuni vitazidi kuwa na nguvu kutokana na damu ya Shahidi Ismail Haniyeh.

Ismail Haniyeh

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imesisitiza katika taarifa yake kwamba, kuuawa shahidi mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas kunaimarisha azma ya wapiganaji wa kambi ya Muqawama ya kukabiliana na adui Mzayuni.  

Hizbullah imesema katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumatano kwamba: Kamanda Shahidi Ismail Haniyeh alikuwa mmoja wa viongozi wakubwa wa Muqawama katika kipindi cha sasa, ambaye alisimama kishujaa dhidi ya mradi wa ubeberu wa Marekani na Wazayuni maghasibu na amesabilia maisha yake kwa ikhlasi na kuuliwa kishahidi.

Tags