Walowezi wa Kizayuni wauvamia tena Msikiti wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i11506-walowezi_wa_kizayuni_wauvamia_tena_msikiti_wa_al_aqswa
Walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wameuvamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa huko Quds Tukufu Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2016 23:11 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni wauvamia tena Msikiti wa al-Aqswa

Walowezi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wameuvamia Msikiti Mtakatifu wa al-Aqswa huko Quds Tukufu Palestina.

Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina kinaripoti kwamba, jana walowezi wa Kizayuni waliendeleza vitendo vyao vya kuyavunjia heshima maeneo matakatifu baada ya kuvamia Masjidul Aqswa.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, walowezi hao wa Kizayuni walikuwa wakisindikizwa na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel na waliingia katika eneo hilo wakipitia upande wa Bab al-Maghariba.

Waumini waliokuweko msikitini hapo kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Swala kwa pamoja walipiga nara dhidi ya Uzayuni na kulalamikia kuingia katika uwanja wa msikiti huo walowezi hao wa Kizayuni.

Hii sio mara ya kwanza kwa walowezi wa Kiyahudi kuuvamia msikiti huo mtakatifu ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vinavyokinzana kabisa na heshima na utukufu wa msikiti huo.

Hatua hizo za kuyavunjia heshima maeneo matakatifu huko Palestina zinakwenda sambamba na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Hujuma hizo na ukandamizaji wa jeshi la Israel zimepelekea kutawanyika cheche za Intifadha mpya huko Palestina.

Itakumbukwa kuwa, tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.