Aug 12, 2024 06:02 UTC
  • Hamas: Vita havitakwisha kama  anavyotarajia adui Muisraeli

Kiongozi  wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, amesema vita "havitakwisha kama anavyotarajia adui Muisraeli."

Osama Hamdan, ambaye ni mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon na pia mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya harakati hiyo, amesema vita vya sasa vya Gaza vitamalizika "kwa maslahi ya muqawama."

Aidha amesisitiza kuwa, "Ikiwa wapatanishi wanataka kukomesha uvamizi, Marekani kwanza lazima iache kuunga mkono utawala wa Kizayuni."

Hamdan aliyasema hayo Jumapili katika mahojiano na televisheni ya Al Manar ya Hizbullah.

Ameongeza kuwa Hamas haitakubali masharti mapya akibainisha kuwa kuna waraka ambao harakati hiyo imeuafiki na inasubiri kutangazwa kwa taratibu za utekelezaji, ikiwa ni pamoja na kusitishwa uvamizi wa Israel, kujiondoa kwake, kufikishwa misaada Gaza na kuzinduliwa mpango wa ujenzi mpya.

Hamas imeripotiwa kukubali pendekezo la Misri na Qatar, ambalo ni pamoja na kusitisha mapigano, kuondolewa kabisa wanajeshi wa Israeli kutoka Gaza, kubadilishana wafungwa, ujenzi mpya wa eneo hilo na kuondolewa mzingiro uliowekwa na utawala wa Israel.

Hali ya Gaza kufuatia hujuma ya Israel

Hata hivyo, Israel imekataa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku waziri mkuu Benjamin Netanyahu akisema kujiondoa kwa vikosi vya uvamizi katika Ukanda wa Gaza "kutawaacha Hamas wakiwa na nguvu."

Kuhusu ripoti kwamba Iran itafanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Israel kutokana na mauaji yake ya kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, Hamdan amesema: “Jibu la Iran ambalo linaweza kuja wakati wowote litaathiri mwenendo wa mapambano na adui."

Tarehe 31 Julai, Israel ikiungwa mkono na Marekani ilimuua Ismail Haniyeh, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Hamas, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian wa Iran.

Kitendo hicho cha kigaidi kilifuatia mauaji mengine ya utawala wa Kizayuni yaliyomlenga Fuad Shukr, kamanda mkuu wa harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah huko Beirut.