Aug 13, 2024 02:34 UTC
  • Utawala wa Kizayuni, mbunifu wa mbinu mpya za mauaji ya kimbari

Katika kitendo kingine cha jinai na uhalifu wa kutisha, utawala wa Kizayuni wa Israel umeshambulia shule ya al-Tabiin huko Gaza na kuuwa shahidi na kujeruhiwa mamia ya Wapalestina.

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), limechapisha taarifa kuhusu shambulio la ndege za kivita za Israel katika Shule ya Al-Tabiin, lililouawa shahidi zaidi ya watu 100 na kujeruhi makumi ya wengine, likitoa wito wa kulindwa shule na makazi ya wakimbizi huko Gaza. UNICEF imetangaza kuwa, zaidi ya asilimia 50 ya shule zinazotumiwa kwa ajili ya kuwapa hifadhi wakimbizi wa Gaza, zimeshambuliwa na utawala wa Kizayuni.

Karibu raia 200 wa Palestina walikuwa wakiswali Swala ya Alfajiri wakati shule hiyo iliposhambuliwa na jeshi la Israel. Katika shambulizi hilo, utawala wa Kizayuni ulitumia mabomu matatu, ambayo kila moja lilikuwa na uzito wa karibu kilo 500.

Mamia ya Wapalestina wameuawa katika shambulizi la Israel, Shule ya al-Tabiin

Baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023 na mafanikio ya makundi ya Muqawama ya Palestina katika vita dhidi ya utawala wa Kizayuni, jeshi la Israel limezidisha mashambulizi yake katika maeneo ya makazi ya raia, hospitali, kambi za wakimbizi na shule; na matokeo ya mashambulizi hayo ya kikatili ni mauaji ya maelfu ya Wapalestina na kujeruhiwa maelfu ya wengine.

Suala muhimu na linalopaswa kumulikwa kuhusiana na mashambulizi hayo ni himaya na misaada isiyo na mpaka ya Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, huku vyombo vya habari vya Magharibi vikiendelea kuhalalisha mauaji hayo ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza na kueneza uwongo wa wanasiasa wao. Baada ya jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni ya kushambulia Shule ya Al-Tabiin, mashirika ya habari ya Marekani, ikiwemo televisheni ya CNN, yanajaribu kuhadaa maoni ya umma kwa habari za kupotosha na kukariri riwaya ya utawala wa Kizayuni kuhusu eti ulazima wa kushambuliwa eneo hilo. 

Licha ya kuwepo ushahidi na nyaraka nyingi kuhusu mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Gaza, utawala huo wa kikatili daima umekuwa ukitoa madai ya uongo kwamba unashambulia maeneo ya wapiganaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas); madai ya uongo ambayo ni udanganyifu unaolenga kuficha jinai za Wazayuni hao huko Palestina.

Ali al-Awar, profesa wa chuo kikuu na mtaalamu wa masuala yanayohusiana na Israel huko Ramallah amesema kuhusu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa kawaida katika hospitali, shule, kambi za wakimbizi ikiwemo shule ya al-Tabiin kwamba: "Israel inaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya taifa letu (Palestina) na kutoa visingizio kuwa wanaouawa katika maeneo hayo ni wapiganaji wa Hamas; hapana, wapiganaji wa Hamas hawapo katika maeneo hayo. Ushahidi wote na video na picha zote zinaonesha waziwazi kuwa waliouawa ni wanawake na watoto wasio na hatia wala ulinzi."

Ripoti ya UNICEF inaonyesha kuwa, kutokana na kukata tamaa na kushindwa kukabiliana na makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina, utawala wa Kizayuni wa Israel umetanguliza mbele vitendo vya kikatili, kutenda jinai na kuendeleza mauaji ya kimbari katika fremu ya malengo yake ya kinyama na ya kutisha.

Mauaji ya umati katika Shule ya al-Tabiin

Faili jeusi la jinai za Wazayuni linazidi kuwa jeusi kuliko hapo awali kutokana na kuendelea vita vya Gaza, na maoni huru ya umma katika ngazi ya kimataifa ambayo yanawaunga mkono watu wa Palestina, katika mikusanyiko yao huko Ulaya, Amerika na sehemu nyingine za dunia yanasisitiza udharura wa kukamatwa na kuhukumiwa viongozi wahalifu wa Israel kama watenda jinai na uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari.

Unyama wa Israel katika shambulizi dhidi ya Shule ya al-Tabiin unalazimu kuwepo umoja na mshikamano mkubwa zaidi wa Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kuwaadhibu Wazayuni maghasibu, na kuwalazimisha waungaji mkono wa Israel huko Marekani na Ulaya kutazama upya matendo yao na himaya na misaada yao kwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanyika huko Gaza. 

Tags