Msikiti wa Al Aqsa wavamiwa na walowezi wakiongozwa na Ben Gvir
Walowezi wa utawala haramu wa Israel wamevamia boma la Msikiti wa al-Aqsa, huku waziri mkaidi mwenye siasa kali za mrengo wa kulia wa utawala huo Itamar Ben-Gvir akijiunga nao na hivyo kuzua mvutano mpya na Waislamu Wapalestina ambao hutekeleza ibada katika eneo hilo takatifu.
Zaidi ya walowezi 1,600 wa Israel, ambao walipangwa katika makundi 13, walivamia Msikiti wa al-Aqsa katika mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel Jumanne asubuhi.
Kwa mujibu wa Idara ya Msikiti wa al-Aqsa, uvamizi wa walowezi katika boma la Msikiti wa al-Aqsa ulikuja kuitikia mwito wa makundi ya Kiyahudi yenye itikadi kali kuhusu maadhimisho ya Tisha B'Av, siku ya kila mwaka ya mfungo wa Kiyahudi ambayo inaashiria kutokea kwa maafa kadhaa katika historia ya Kiyahudi.
Idara hiyo imeripoti kuwa, vikosi vya Israel viliwazuia waumini kuingia katika ua wa Msikiti wa al-Aqsa ili kuwezesha uvamizi wa walowezi katika eneo hilo takatifu la Kiislamu. Hatua hiyo ililisababisha mapigano na waumini wa Kipalestina.
Video za mitandao ya kijamii zinaonyesha walowezi wa Kizayuni waliokuwa wanalindwa na askari katili wa Israel wakiwashambulia waumini wa Kipalestina.
Walowezi hao waliingia katika msikiti huo kupitia lango la magharibi la al-Mugharibah, njia ambayo hutumika mara kwa mara wakati wa uvamizi huo, huku wakiinua bendera ya utawala bandia wa Israel ndani ya lango la al-Salsila kwenye Msikiti wa al-Aqsa.
Waziri wa mrengo wa kulia wa Israel Itamar Ben-Gvir, akiandamana na waziri mwenzake Yitzhak Wasserlauf, walishiriki katika uvamizi huo.
Ben-Gvir, ambaye ni msimamizi wa polisi ya Israel, amekuwa akisisitiza mara kwa mara kwamba anaamini Wayahudi wanapaswa kuruhusiwa kutekeleza ibada zao katika msikiti huo mtakatifu, kinyume na sheria inayosimamia Msikiti wa al-Aqsa.