Uwezo wa kisiasa wa matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s)
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115450-uwezo_wa_kisiasa_wa_matembezi_ya_arubaini_ya_imamu_hussein_(a.s)
Mamilioni ya watu kutoka nchi tofauti wanashiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s).
(last modified 2024-08-20T23:00:08+00:00 )
Aug 20, 2024 23:00 UTC
  • Uwezo wa kisiasa wa matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s)

Mamilioni ya watu kutoka nchi tofauti wanashiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s).

Matembezi haya yana nafasi na uwezo mkubwa na muhimu wa kisiasa.

Katika miaka ya hivi karibuni, maadhimisho ya matembezi ya Arubaini yamekuwa jambo la kipekee ambalo limesababisha ulimwengu kushangaa juu ya jambo hili kubwa.

Mkusanyiko huu mkubwa wa kibinadamu umekuwa ukitazamwa kama mtaji wenye fursa nyingi za kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi ambazo zimepuuzwa katika matukio mengi.

Mojawapo ya fursa muhimu za kipekee za mkusanyiko huu wa watu, ni kutumiwa uwezo wake wa kisiasa. Uwezeshaji, umoja na mshikamano na kuimarisha roho ya pamoja ni kati ya utendaji wa kisiasa wa mashaya na matembezi ya Arubaini ya Imamu Hussein (a.s).

Moja ya uwezo wa kisiasa wa matembezi ya Arubaini ni kuonyesha tena mfungamano wa kihistoria wa mataifa mawili ya Iran na Iraq. Ingawa uhusiano kati ya Iran na Iraq umekumbwa na misukosuko mingi katika nyakati tofauti za kihistoria, lakini mizizi ya kiutamaduni na ustaarabu kati ya mataifa hayo mawili ni mikongwe na ina historia ndefu.

Kutokana na kuwepo kwa maingiliano ya kiustaarabu na kiutamaduni ambapo mazuwwari wa Iran na Iraq hutembelea mataifa haya mawili kwa ajili ya kufanya ziara katika maeneo matakatifu, kumekuwa na mfungamano wa kihuba, kihisia na kiutamaduni kati ya mataifa haya mawili.

 

Uwezo mwingine wa kisiasa wa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s) ni kuonyesha uwezo wa kambi ya muqawama katika kusimamia nidhamu ya kikanda. Matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein, ambayo yaliundwa kwa msingi wa mvuto wa kiutamaduni na kukita mizizi katika imani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, yamegeuka na kuwa moja ya vielelezo vya nguvu laini ya mazungumzo ya Shia katika ulimwengu wa Kiislamu na mfumo wa kimataifa, ambapo, pamoja na utendaji wake wa kimaingiliano na kuunda umoja, yanaweza pia kuwa na utendaji mbalimbali wa kisiasa kwa minajili ya mamlaka ya kisiasa.

Kufanyika matembezi ya Arubaini ya Imam Huseein yakiwa na mahudhurio ya zaidi ya watu milioni ishirini, licha ya vitisho vya makundi vya kisalafi na kitakfiri, kunatoa ujumbe maalumu wa kisiasa na kimkakati kwa nchi zinazounga mkono makundi haya, ambazo zilijaribu kutumia nyenzo zao kwa ajili ya  kubadilisha mlingano wa nguvu na madaraka kwa ajili waungaji mkono wao.

 

Uwezo mwingine wa kisiasa wa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s) ni kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophbia) na chuki dhidi ya Iran (Iranophobia). Matembezi ya Arubaini ya Imam Husseiin (a.s), bila kujali kwamba, yana nembo ya Ushia au Usuni, ni alama nzuri na ya kibinadamu inayotokana na utamaduni wenye muelekeo wa Kiislamu. Kwa hakika matembezi haya yanaonyesha kuwa, tofauti na propaganda na hata  itikadi za wenye msimamo mikali ya Kisalafi na Kiwahabii, Uislamu ni dini ya upendo na huruma.

Arubaini ya Imamu Hussein ni wakati ufaao zaidi wa kuisafisha sura ya Uislamu kutokana na usomaji wa kitaasubi, kichuki, kiitikadi kali na wa kikatili wa Waislamu ambao, kwa kuendeleza mafundisho yao ya kufurutu ada ya Kisalafi na Kiuwahabi, wametoa pigo kubwa kwa utambulisho wa kupenda amani lakini wa kupinga dhulma wa Uislamu safi wa Muhammad (SAW).

Kwa sababu vuguvugu hili la amani, ambalo halina chochote isipokuwa ujumbe wa wema, amani, utulivu na huruma, linasambaratisha mipango michafu ya madola makubwa ya kuonyesha sura mbaya ya Uislamu na madhehebu ya Shia.