Muqawama wa Iraq watumia droni za kamikaze kupiga Haifa
(last modified Wed, 04 Sep 2024 07:00:03 GMT )
Sep 04, 2024 07:00 UTC
  • Muqawama wa Iraq watumia droni za kamikaze kupiga Haifa

Harakati ya Muqawama ya Iraq imefanya shambulizi la ndege zisizo na rubani dhidi ya mji wa Haifa, kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kundi hilo la Muqawama limetangaza leo Jumatano kuwa, limeshambulia mji bandari wa Haifa kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kwa kutumia droni za kamikaze mapema asubuhi.

Harakati ya Muqawama ya Iraq imeeleza bayana kuwa, operesheni hiyo ya leo asubuhi ni katika mfululizo wa mashambulizi ya kulipiza kisasi cha jinai zinazofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Muqawama wa Iraq umesema kuwa, umeshambulia kwa droni bandari ya Haifa, kambi na maeneo ya kistratajia ya jeshi la Israel ikiwa ni sehemu ya kupigana bega kwa bega na wanamapambano wa Palestina wanaokabiliana na mashambulizi ya kila upande ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Bandari ya Haifa yashambulia kwa droni za wanamuqawama

Makundi ya Muqawama ya Iraq, Palestina na Yemen yaliingia vitani kushambulia maeneo muhimu sana ya Israel baada ya utawala huo katili ambao unaungwa mkono kwa hali zote na Marekani na madola mengine ya kibeberu ya Magharibi, kuzidisha jinai zake dhidi ya wanawake na watoto wadogo pamoja na wazee na raia wa kawaida huko Palestina hasa Gaza.

Katika mikakati na stratijia zake mpya, kambi ya Muqawama ya Iraq imeamua sasa kuzidisha mashambulizi yake dhidi ya maeneo muhimu ya utawala wa Kizayuni yakijumuisha pia viwanja vya ndege na kambi za kijeshi za Israel ili kuulazimisha utawala huo ukomeshe jinai zake dhidi ya Wapalestina.