UNICEF: Chanjo ya polio huko Gaza ni mojawapo ya kampeni hatari zaidi duniani
(last modified Thu, 05 Sep 2024 02:32:25 GMT )
Sep 05, 2024 02:32 UTC
  • UNICEF: Chanjo ya polio huko Gaza ni mojawapo ya kampeni hatari zaidi duniani

Shirika la Kuhudimia Watoto la Umoja wa Mataifa la (UNICEF) limesema zoezi la kutoa chanjo ya polio kwa watoto wa Kipalestina katika eneo la Ukanda wa Gaza lilikuwa miongoni mwa kampeni ngumu na hatari zaidi duniani licha ya kusitishwa kwa muda mapigano katika eneo hilo kwa ajili ya zoezi hilo.

Shirika hilo lilisema jana Jumatano kwamba zaidi ya timu 500 zilitumwa katikati mwa Gaza wiki hii, kutoa chanjo kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 10. UNICEF imesema, kampeni hiyo iliwafikia watoto 189,000, na kuvuka lengo lake na kutoa chanjo hiyo kwa watoto wa eneo hilo linalozingirwa na Wazayuni la Palestina.

UNICEF imesema kwamba Gaza, iliyoharibiwa na vita vya miezi 11 vya Israel, "tayari ni mahali hatari zaidi duniani kuwa mtoto, na licha ya kusitishwa mashambulizi ya Israel kwa ajili ya chanjo ya polio, kampeni ya kutoa chanjo inakabiliwa na hatari kubwa na vikwazo visivyoweza kufikirika, ikiwa ni pamoja na barabara zilizoharibika na kubomolewa miundombinu ya afya, watu waliokimbia makazi yao, uporaji na kuvurugwa njia za usambazaji.

Gaza

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kwamba awamu ya kwanza ya kampeni yake ya chanjo kwa watoto wa katikati mwa Gaza ilikamilika jana Jumatano.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema "ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa kupata chanjo", timu za madaktari zitaendelea kutoa chanjo katika "maeneo manne maalumu" katikati mwa Gaza kwa siku tatu zaidi.

Wataalamu wa afya wanasema uharibifu uliofanywa na Israel wa miundombinu ya afya na usafi wa mazingira katika eneo hilo umekuwa chanzo cha mlipuko wa ugonjwa hatari wa polio.