Israel yafanya mashambulizi ya kipunguani kusini mwa Lebanon
Ndege za utawala wa Kizayuni zimefanya mashambulizi ya kiwendawazimu na kipunguani kwa muda wa saa mbili mfululizo katika maeneo kadhaa ya kusini mwa Lebanon.
Televisheni ya al Manar ya Lebanon imetangaza habari hiyo na kusema kuwa, ndege za Israel zimefanya mashambulizi kwa takriban masaa mawili hadi leo alfajiri kwa kushambulia maeneo 14 ya kusini mwa Lebanon.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, vitongoji vya kusini mwa Lebanon vya Kfarhamam, Tayr Harfa, Zawtar, al Salhani, Ramiya, Deir Siriane, Zibqine, Chihine, Jibbain na Yater vimeshambuliwa kiwendawazimu na ndege za utawala wa Kizayuni kwa takriban saa mbili mfululizo.
Maeneo mbalimbali ya Lebanon hususan ya kusini mwa nchi hiyo yamekuwa yakishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege za kivita za Israel kutokana na maeneo hayo kujitolea muhanga kuwatetea ndugu zao wa Ghaza wanaoshambuliwa kinyama na utawala wa Kizayuni hivi sasa.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeingia vitani kupambana na utawala wa Kizayuni kama sehemu ya kuwaunga mkono ndugu zao Wapalestina na inafanya mashambulizi ya mara kwa mara hasa katika maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina la kupanga la Israel.
Mara kwa mara Hizbullah ya Lebanon inatangaza kuwa, inafanya mashambulizi hayo kuonesha jinsi ilivyo bega kwa bega na wananchi wa Palestina na wanamapambano wa Palestina na itaendelea na mashambulizi hayo hadi utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake huko Ghaza.