Wazayuni waendelea kuangamizwa katika operesheni za kulipiza kisasi
Kwa akali walowezi watatu wa Kizayuni wenye umri wa makamo wameangamizwa katika operesheni ya kulipiza kisasi karibu na kivuko daraja la Karama (Allenby) kwenye mpaka kati ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu na Jordan, huku mashambulizi ya anga ya Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza unaozingirwa yakiendelea.
Huduma ya ambulensi ya Magen David Adom ya Israel awali ilisema iliwatibu watu hao katika eneo la tukio, kabla ya kulazimika kukiri na kutangaza vifo vyao hapo baadaye.
Vyombo vya habari vya Kizayuni vimewanukuu wahudumu wa shirika hilo la ambulensi wakidai kuwa, “Tulikuta wanaume watatu wakiwa wamepoteza fahamu, hawana mapigo ya moyo na hawapumui, wakiwa na majeraha ya risasi."
Pamoja na timu ya matibabu ya jeshi la Israeli, tulifanya juhudi za kuwafufua, lakini kwa bahati mbaya, tulilazimika kutangaza vifo vyao kwenye eneo la tukio," limetangaza shirika hilo katika taarifa.
Mamlaka za Israel na Jordan zimetangaza kuwa, kivuko cha Allenby kimefungwa kwa muda usiojulikana, kufuatia tukio hilo la kulipiza kisasi katika eneo hilo la Wapalestina linalokaliwa kwa mabavu.
Wiki iliyopita, askari polisi wawili wa Israel na mlowezi mmoja wa Kizayuni waliangamizwa katika operesheni nyingine ya kulipiza kisasi karibu na mji wa al-Khalil, katika eneo la Ukingo wa Magharibi.
Aidha kabla ya hapo, vyombo vya habari vya Kizayuni viliripoti kuwa, kamanda mmoja wa jeshi la Israel ameuawa wakati wa shambulizi la utawala huo katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.