Utawala wa Kizayuni waua kigaidi makamanda 3 wa chama cha PLO
Shambulio la kigaidi ambalo limetekelezwa na utawala wa Kizayuni katika eneo la "Al-Kola" mjini Beirut, Lebanon limepelekea kuuawa shahidi makamanda watatu waandamizi wa chama cha Ukombozi wa Palestina PLO.
PLO imethibitisha habari ya kuuawa makamanda wake hao na kutangaza majina ya waliouawa shahidi katika shambulio hilo la kigaidi katika eneo la Al-Kula.
Mohammed Abdul Aal, mjumbe wa ofisi ya kisiasa na mkuu wa idara ya kijeshi na usalama ya chama hicho, ni mmoja wa waliouawa katika shambulio hilo la kinyama lililofanywa na utawala wa Israel.
Emad Oudeh na "Abdul Rahman Abdul Al, ni makamanda wengine wawili wa PLO waliouawa kigaidi na utawala huo wa Kizayuni.
Watu wengine 10 pia wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililofanyika dhidi ya hengo moja karibu na daraja la al-Kola.
Wizara ya Afya ya Lebanon, ilitangaza Jumapili usiku kwamba mashambulizi hayo ya kikatili ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon mjini Beirut yamepelekea watu 109 kuuawa katika muda wa saa 24 zilizopita.
Wizara hiyo vile vile imetangaza kuwa watu wengine 364, walijeruhiwa katika shambulio hilo la Jumapili.