UNICEF yaeleza wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya watoto wa Lebanon
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu nchini Lebanon na ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya watoto nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Catherine Russell, ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba, watoto wasiopungua 80 wameshauawa shahidi na mamia ya wengine kujeruhiwa kutokana na mashambulizi makali ya utawala wa Kizayuni nchini Lebanon yaliyoanza wiki iliyopita.
Ameashiria kuongezeka mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Lebanon katika siku za hivi karibuni na kusema kuwa, katika muda wa wiki moja tu, zaidi ya watu milioni moja wakiwemo watoto laki tatu wa Lebanon wamekimbia makazi yao.
Siku ya Jumatatu ya tarehe 23 Septemba 2024, jeshi la utawala wa Kizayuni lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon, mashambulizi ambayo yanaendelea hadi hivi sasa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon, zaidi ya watu 800 wameshauwa shahidi na takriban watu 3000 wameshajeruhiwa kutokana na mashambulizi makubwa ya jeshi la utawala dhalimu wa Israel huko Lebanon.
Vile vile Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto amesema kuwa, watoto wengi katika Ukanda wa Ghaza wamekumbwa na utapiamlo na wako katika ukingo wa kifo.
Hapo awali pia duru za Wapalestina zilikuwa zimetangaza kuwa, watoto wachanga na watoto wadogo wa Kipalestina wanaendelea kufariki dunia kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza kutokana na utapiamlo na ukosefu wa maji safi ya kunywa.