Umuhimu maradufu wa kikao cha Doha, kwa kuzingatia hali ya eneo
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameshiriki katika kikao cha Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) huko Doha Qatar, ambapo masuala yanayohusiana na hali iliyosababishwa na mashambulizi na mauaji ya kigaidi ya mara kwa mara ya utawala wa Kizayuni katika eneo na jibu kali la Iran dhidi yake, yana umuhimu wa kujadiliwa na kufanyiwa mashauriano na serikali za eneo hili.
Rais Pezeshkian amesema safari yake mjini Doha imefanyika kwa malengo mawili moja likiwa ni kujadiliana na viongozi wa serikali ya Qatar kuhusu maingiliano ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii ya pande mbili, ambayo yamepelekea kusainiwa hati za maelewano, na la pili ni kujadili hali ya eneo na jinsi nchi za Kiislamu zinapaswa kushirikiana kwa ajili ya kushughulikia na kutatua changamoto zilizopo.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa kikao hicho kimefanyika kwa madhumuni ya kuushinikiza utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake la sivyo ikabiliwe na radiamali kali ya nchi za Kiislamu. Kile kinachoongeza maradufu umuhimu wa kikao cha Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) mjini Doha ni kwamba, nchi za eneo hazijawahi kukutana tangu kuanza duru mpya ya mashambulizi na jinai za Israel dhidi ya Lebanon na kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbollah nchini Lebanon, ambako kulitimia kwa kutumia mabomu ya kulipua miamba yaliyotolewa na Marekani kwa utawala huo wa kigaidi, ambapo ombi lililotolewa na Kiislamu ya Iran la kufanyika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC bado halijajibiwa. Hii ni pamoja na kwamba, chokochoko za Netanyahu sio tu zinalenga mhimili wa muqawama, bali zinahatarisha usalama wa eneo na ulimwengu mzima.
Kwa maelezo hayo na kwa kuzingatia kuwepo baadhi ya viongozi wa nchi za eneo katika Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia, kikao cha Doha nchini Qatar kinatoa fursa ya maafikiano na uratibu baina ya nchi za Kiislamu za eneo ili kukabiliana na uchochezi wa vita wa utawala wa Kizayuni na hasa Netanyahu mwenyewe huku kikifuatilia ajenda zake za kawaida.

Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD), linajumuisha nchi 35 za Asia, ambazo zimekuwa zikiendeleza mazungumzo kuhusu Asia kwa zaidi ya miaka 20 kwa lengo la kutekeleza miradi na mipango mbalimbali ya ushirikiano katika nyanja tofauti za kiuchumi na kiutamaduni.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mwenyekiti wa kongamano hili tangu mwezi Oktoba mwaka jana, ambapo kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa jukwaa hili kilifanyika chini ya uenyekiti wa Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, pembeni mwa kikao cha karibuni cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Malengo makuu ya Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia yanaweza kufupishwa katika kukuza ushirikiano wa nchi za Asia kwa shabaha ya kupunguza umaskini na kuboresha hali ya maisha ya watu wa Asia. Bara la Asia lina suhula na fursa nyingi za kufikia maslahi ya pamoja na kuundwa ulimwengu bora na wa kibinadamu zaidi kwa kunufaika na masuala kama vile idadi kubwa ya watu na maliasili zilizopo. Hali kadhalika utamaduni, dini na mila tofauti za mataifa ya Asia ni mojawapo ya mambo yanayoweza kuharakisha uimarishwaji wa ushirikiano na ustawi wa kifikra kati ya mataifa ya eneo hili.

Jukwaa la Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia ni nyenzo muhimu na yenye thamani kubwa katika uwanja huu. Jukwaa hili linaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuunda Asia yenye umoja, yenye nguvu na yenye taathira zaidi. Asia inaunda asilimia 45 ya pato jumla kimataifa, suala ambalo linaonyesha wazi ushirikiano na umoja uliopo kati ya nchi za eneo hili.
Masuala muhimu kama vile kutofanya kazi kwa baadhi ya mifumo ya kimataifa, uharibifu na ghasia zinazoibuliwa na baadhi ya mataifa yenye nguvu duniani, umaskini, dhulma, mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, uhaba wa usalama wa chakula, nishati, majanga ya asili na masuala kama haya yanaashiria ulazima wa kubuniwa mbinu mpya za kukabaliana nayo barani Asia.
Katika miongo miwili iliyopita, viongozi wa nchi wanachama wa Jukwaa la Mazungumzo la Asia wamezingatia kwa usahihi umuhimu wa kuunda jumuia ya Asia. Bara kongwe la Asia tangu miongo mingi huko nyuma, limekosa kuwa na utaratibu wa kina wa kushughulikia changamoto za eneo hili na kimataifa. Hii leo inaonekana kuwa wakuu wa jukwa la ADC wamezingatia zaidi umuhimu wa kuzipa kipaumbele juhudi za kubuni Jumuiya ya Asia ambayo itaweza kuyashughulikia vizuri masuala ya nchi wanachama. Kuhusiana na hili, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa mwanachama muhimu na hai wa Jukwaa la Ushirikiano wa Asia (ACD), daima imekuwa ikijaribu kuimarisha maingiliano chanya ya pande mbili na ya pande kadhaa kati ya nchi wanachama wa jumuiya hii muhimu.