Khalid Mash'al: Kuuawa shahidi Yahya al-Sinwar hakutasimamisha muqawama
(last modified 2024-10-22T02:24:30+00:00 )
Oct 22, 2024 02:24 UTC
  • Khalid Mash'al: Kuuawa shahidi Yahya al-Sinwar hakutasimamisha muqawama

Khalid Mash'al, afisa mwandamizi na Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS nje ya Gaza amesema kuwa, kuuawa shahidi Yahya al-Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati hiyo hakutasimamisha muqawama na mapambano ya Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. 

Kiongozi huyo wa ngazi za juu wa HAMAS amesisitiza kuwa, muqawama na mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel yataendelea mpaka utakapopatikana ushindi na ukombozi wa Palestina.

Mash'al ameongeza kuwa, wakati wa kujiri vita baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqswa, Hamas imepoteza idadi kubwa ya viongozi wakubwa wa harakati hiyo huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, nje ya nchi na wakaazi wa kambi hizo, na daima imekuwa ikiwatoa viongozi wake katika njia ya kuuawa shahidi, fahari, ukombozi wa ardhi na uhuru kutoka katika mikono ya wavamizi wa Israel.

Shahidi Yahya al-Sinwar mkuu wa zamani wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS

 

Kadhalika amesema, tangu kuasisiwa kwake, Hamas imepoteza viongozi wengi akiwemo Ahmad Yasin waliouawa katika njia ya mapambano na muqawama dhidi ya Israel na mauaji hayo hayajatia dosari azma na irada ya muqawama wa Palestina.

Yahya al Sinwar Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) aliuawa shahidi Jumatano iliyopita akipambanana adui Mzayuni katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.