Wanajeshi wa Israel wapata pigo jingine Ghaza
Licha ya kupita miezi kadhaa ya uhalifu na jinai za kivita huko Ghaza baada ya Israel kuvunja makubaliano ya amani na kuanzisha upya mashambulizi, lakini bado wanamapambano wa Palestina wako kwenye mstari wa mbele wa mapambano na wanaendelea kutoa vipigo kwa wanajeshi vamizi wa Israel.
Mapema leo Jumapili duru za habari za utawala wa Kizayuni zimeripoti kujeruhiwa askari kadhaa wa Israel na kuhamishiwa kwenye hospitali za Tel Hashomer na Belenson.
Kwa mujibu wa duru hizo, wanajeshi wa Israel waliojeruhiwa huko Ghaza wamesafirishwa hadi kwenye vituo vya matibabu kwa helikopta za kijeshi kutokana na mapigano yanayoendelea katika Ukanda wa Ghaza.
Tovuti ya habari ya Hadashot Bazman imeripoti maafa mengine waliyopata wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Ghaza, tena kwenye maeneo ambayo utawala wa Kizayuni unadai umeyadhibiti. Lakini hadi wakati tunaandaa taarifa hii, kulikuwa hakujatolewa maelezo zaidi kuhusu habari hiyo.
Matukio hayo yanakwenda sambamba na kuingia brigedi zote za askari wa miguu na wenye silaha za jeshi la utawala huo ghasibu katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa mtandao wa Hebrew Kan, kikosi cha askari wa miavuli cha Israel pia kimetumwa kikamilifu kwenye eneo hilo katika muda wa saa 24 zilizopita na kimeingia kwenye operesheni hiyo ikiwa ni uthibitisho mwingine kuwa mapambano makali yanaendelea hasa kaskazini mwa Ghaza.
Israel imeongeza jinai zake za kijeshi huko Ghaza huku dunia nzima ikiendelea kuulaani utawala wa Kizayuni kwa uhalifu wake mkubwa wa kivita dhidi ya watu wasio na ulinzi wa Ukanda wa Ghaza.