Mkutano wa kuadhimisha Siku ya Afrika wafanyika Addis Ababa
Mkutano wa kuadhimisha Siku ya Afrika ulifanyika katika makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) huko Addis Ababa, Ethiopia, siku ya Jumamosi.
Tukio hilo lilikuwa la kuadhimisha miaka 62 tangu kuanzishwa kwa Muungano wa Afrika (OAU), ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).
Mahmoud Ali Youssouf, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), alitoa hotuba akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu: “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia.” Alizungumzia kuhusu “uhalifu uliofanyika wakati wa biashara ya utumwa na ukoloni dhidi ya mamilioni ya Waafrika.”
“Ingawa haki na fidia zimechelewa kwa muda mrefu,” Youssouf alisema, “Afrika haitafungwa mateka na maumivu ya yaliyopita.” Aidha amesema: “Afrika inaendelea kujitolea na kupambana kwa ajili ya uhuru dhidi ya migogoro, hali ya kutoendelea na vita. Bara linaendelea kujenga mustakabali wa amani, ustawi na mshikamano."
Pia amesema faida kuu za kimkakati za Afrika ni idadi kubwa na inayoongezeka ya vijana, ardhi yenye rutuba, utajiri wa madini na uwezo wa kuzalisha nishati mbadala. Kwa idadi ya watu inayotarajiwa kuzidi bilioni 2.5 ifikapo mwaka 2050. Youssouf amesisitiza kuwa Afrika si tu ni bara la baadaye bali pia ni injini ya mageuzi ya kimataifa.
Amehitimisha kwa kusema: “Ni jukumu letu kama Waafrika kulinda rasilimali zetu na kuziweka thamani kupitia miradi ya mabadiliko kama vile Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA). Afrika haipaswi tena kuachwa nyuma katika masuala ya kisiasa ya dunia."

Siku ya Afrika huadhimishwa kila mwaka duniani kote tarehe 25 Mei. Huko nyuma ilijulikana kama Siku ya Uhuru wa Afrika au Siku ya Ukombozi wa Afrika, ikiwa ni kumbukizi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (OAU) na nchi 31 huru mnamo tarehe 25 Mei 1963. Kwa sasa, AU ina wanachama 55 wa mataifa huru, wanaofanya kazi kwa kuzingatia dhana ya “Afrika Iliyoungana, Yenye Ustawi na Amani, Inayoendeshwa na Wananchi Wake na Kuwa Nguvu Hai Katika Medani ya Dunia.”
Malengo ya taasisi hiyo ni pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano, kukuza ushirikiano kati ya mataifa ya Afrika, kulinda uhuru na mipaka ya wanachama, kutokomeza kila aina ya ukoloni, kuzuia kuingiliwa masuala ya ndani ya mataifa na kutatua migogoro kwa njia ya amani.
Kila mwaka kabla ya Siku ya Afrika, AU huchagua kaulimbiu inayoiona kuwa na umuhimu mkubwa. Wakati mwaka 2024 ulikuwa umetengwa kwa maendeleo ya elimu na ujuzi barani Afrika, mwaka huu kaulimbiu ya “Haki kwa Waafrika na Watu wa Asili ya Kiafrika Kupitia Fidia” inalenga kuheshimu kumbukumbu ya walioteseka chini ya utumwa na ukoloni.