Hizbullah: Trump amenasa kwenye minyororo ya Israel, anapasa kujikomboa
Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah, Sheikh Naim Qassem amesema kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump anapasa kujikomboa kutoka katika "mikono ya Israel ikiwa anataka kufikia malengo yake."
Sheikh Qassem aliyasema hayo jana Jumapili wakati wa hotuba yake aliyoitoa kwa mnasaba wa Siku ya Muqawama na Ukombozi, ambapo pia ameeleza kuwa, Trump anapaswa kuchangamkia fursa hiyo na kujitua mzigo- ambao ni Israel.
"Marekani inakiuka mamlaka ya kitaifa ya kujitawala Lebanon, na haitaweza kuweka masharti ya uvamizi huo, bila kujali gharama ya kujitolea mhanga na makabiliano," amesema.
Sheikh Qassem alianza hotuba yake kwa kusema kwamba Muqawama umebadilika kutoka mradi na kuwa nguzo ya kudumu ya Lebanon kufuatia kufukuzwa kwa utawala wa Israel Mei 24, 2000.
"Muqawama ndilo chaguo pekee la ukombozi," amesisitiza mwanachuoni huyo mashuhuri wa Lebanon na kueleza kuwa, "Muqawama ulitokana na hitaji la kukabiliana na vitisho na ni msaada wa asili kwa jeshi."
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amebainisha kuwa, kuibuka kwa Muqawama huo ni jibu la asili kutoka kwa watu wenye izza wasiokubali kudhalilishwa, kukaliwa kimabavu na kujisalimisha kwa adui Mzayuni.
"Muqawama huo uliibadilisha Lebanon kutoka hali ya udhaifu hadi hali ya nguvu na izza, na kukomesha matarajio ya Israel ya kujitanua," ameongeza Sheikh Qassem.
Amebainisha kuwa, "Muqawama umeleta mabadiliko nchini Palestina, umeweka adui kwenye njia ya kuporomoka, na kuandaa mazingira kwa maendeleo yote yaliyofuata."