Walimwengu waendelea kutoa wito wa kuhitimishwa mzingiro Gaza
(last modified Mon, 26 May 2025 02:20:24 GMT )
May 26, 2025 02:20 UTC
  • Walimwengu waendelea kutoa wito wa kuhitimishwa mzingiro Gaza

Huku hali mbaya ya kibinadamu ikiongezeka katika Ukanda wa Gaza, ripoti zinaonyesha kuwa Israel imewaua zaidi ya watoto 14,500 wa Kipalestina hadi sasa, kwa risasi, makombora, au kufunikwa chini ya vifusi.

Umoja wa Mataifa unaonya kuwa idadi hii inaweza kuongezeka maradufu, huku watoto wengine 14,000 wakitarajiwa kufa kwa njaa ikiwa Israel haitakomesha mashambulizi yake ya kijeshi na kuondoa kizuizi cha misaada.

Janga hili la kibinadamu haliwezi kustahimilika, huku Israel ikiendelea kuzuia chakula, dawa, na mafuta kuwafikia watoto wanaowategemea misaada hiyo kwa ajili ya maisha yao.

Hali hii imezua shutuma nyingi kutoka kwa jamii ya kimataifa, ambayo inashuhudia wazi ukweli huu. Licha ya walimwengu na mataifa mbalimbali kutoa mwito wa kuhitimishwa mzingiro wa Gaza, lakini Israel ikipata himaya na uungaji mkono wa Marekani na washirika wake. Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, uhaba mkubwa wa chakula katika Ukanda wa Gaza umefikia kiwango cha janga la njaa.

Mtandao wa Kimataifa wa Kupambana na Migogoro ya Chakula umetangaza kuwa uhaba mkubwa wa chakula huko Gaza umefikia kiwango kibaya zaidi cha "janga na njaa." Wakati huo huo, Philippe Lazzarini Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na kusisitiza kuwa kuzingirwa eneo hilo na utawala wa Kizayuni kunakwamisha misaada ya kibinadamu kuingia katika hilo; kwa hiyo wakazi wa eneo hilo wapo kwenye ukingo wa njaa.