Kwa nini Trump ana vigezo vya kibaguzi kuhusu suala la nyuklia?
(last modified Mon, 26 May 2025 02:14:10 GMT )
May 26, 2025 02:14 UTC
  • Kwa nini Trump ana vigezo vya kibaguzi kuhusu suala la nyuklia?

Siku ya Ijumaa, Mei 23, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini dikri mpya kadhaa zinazolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji wa nishati ya nyuklia, kupunguza kanuni za udhibiti na kupanua sekta ya urutubishaji wa madini ya urani nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo anaendelea kuziwekea nchi nyingine hasa Iran, vikwazo katika uwanja huo na kuzitaka zisimamishe urutubishaji urani. Akizungumza karibuni mbele ya wakurugenzi wakuu wa makampuni yanayofanya kazi katika sekta ya nyuklia, Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi na Doug Burgum, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani Trump alisema: "Hii ni sekta inayong'ara. Ni lazima mjishughulishe ipasavyo kwenye sekta hii." Doug Burgum aliongeza kwa kusema kwamba hatua ya Trump katika uwanja huo "imelegeza sheria ngumu zilizowekwa miaka 50 iliyopita katika sekta ya nyuklia."

Maafisa wa Ikulu ya White House wanadai kwamba hatua hii itafungua njia ya "kudhamini umeme salama na wa kutegemewa katika vituo muhimu vya ulinzi na vya takwimu za Akili Mnemba." Afisa mmoja wa serikali ya Marekani alisema kabla ya kutiwa saini maagizo hayo kwamba lengo la kujenga vinu zaidi vya nyuklia ni kukidhi mahitaji ya nishati yanayoongezeka kila siku kutokana na maendeleo ya teknolojia ya Akili Mnemba.

Katika maagizo hayo, Trump ameitaka Tume Huru ya Marekani ya Kudhibiti Nyuklia (NRC) kulegeza masharti magumu na kuharakisha mchakato wa kutoa leseni kwa ajili ya kujengwa vinu vya nyuklia na vya kuzalisha nishati ya nyuklia. Maagizo hayo pia yanajumuisha mapitio ya viwango vya wafanyakazi wa Tume ya Udhibiti wa Nyuklia na ushirikiano kati ya Wizara za Nishati na Ulinzi za Marekani ili kujenga vinu vya nyuklia kwenye ardhi ya serikali ya shirikisho.

Malengo mengine ya maagizo hayo ya kiutendaji ni pamoja na kurekebisha utafiti wa nishati ya nyuklia katika Wizara ya Nishati, kubuni mkakati wa kujenga vinu vya nyuklia kwenye ardhi inayodhibitiwa na serikali, mageuzi ya kina katika Tume ya Kudhibiti Nyuklia (NRC), na kupanua uchimbaji na urutubishaji wa urani nchini Marekani. Trump pia ametoa maagizo ya kuongezwa uchimbaji wa urani ndani ya nchi na kuimarisha uwezo wa kurutubisha urani.

Donald Trump

Kama ilivyokuwa katika muhula wake wa kwanza, Donald Trump ameendeleza mipango ya kuimarisha uwezo wa nyuklia wa Marekani katika muhula wake wa pili, ambapo ametenga bajeti kubwa kwa ajili hiyo. Isisahaulike kwamba tangu urais wa Barack Obama, Marekani imeendelea na mchakato wa kujenga upya, kusasisha, na kuongeza uwezo wake wa kimkakati wa nyuklia, huku ikitumia mamia ya mabilioni ya dola kwa lengo hilo.

Ili kuhalalisha jambo hilo, Pentagon imeashiria upanuzi wa maghala ya nyuklia ya mahasimu wa Marekani na kutumia kisingizio hicho kutazama upya na kuimarisha mipango yake ya nyuklia, kwa ajili eti ya kukabiliana na vitisho vinavyoweza kutoka upande wa Russia na Uchina.

Jambo muhimu katika uwanja huu ni kwamba kwa kuimarisha mipango yake ya nyuklia, Marekani imepuuza mikataba na maazimio muhimu ya kimataifa kuhusiaa na silaha za nyuklia, ukiwemo Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na wakati huo huo kutuhumu na kuzishinikiza nchi nyingine, ikiwemo Iran, ambazo zinaendeleza mipango ya nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Wakati maendeleo ya nyuklia ya Iran ni ya amani kabisa, Marekani, washirika wake wa Magharibi na utawala haramu wa Israel wanaituhumu Tehran kuwa inaendesha mpango wa nyuklia kwa malengo ya kijeshi. Kwa miaka mingi, nchi za Magharibi zimeituhumu Iran kuwa ina mpango wa kijeshi wa nyuklia na hivyo kuiwekea vikwazo vikali, bila kutoa ushahidi wowote wa kuaminika. Haya yanajiri pamoja na kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa, sio tu kwamba haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia, bali hata haifikirii kuelekea upande huo. Tuhuma za Washington dhidi ya Tehran kuhusiana na suala la nyuklia, kwa hakika zinaonyesha hofu iliyonayo Marekani kuhusu kuimarika nguvu ya kitaifa ya Iran katika nyanja mbalimbali.

Kinyume na madai yasiyo na msingi ya nchi za Magharibi, Iran imeweza kutumia teknolojia ya amani ya nyuklia katika maeneo ya uzalishaji umeme, dawa, kilimo na nyanja nyinginezo. Uundaji wa vinu vya nyuklia umewekwa kwenye ajenda ya kazi ya Iran kwa kuzingatia hitajio lake kubwa la umeme na mahitaji mengine ya kiraia. Kuhusu hilo, Pejman Shirmardi, Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema: "Iran imepata kujitosheleza katika uzalishaji wa zana za teknolojia ya nyuklia." Mafanikio hayo ya Shirika la Nishati ya Atomiki bila shaka ni turufu kwa timu inayofanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani. "Wasiwasi mkubwa wa upande wa Magharibi ni kuhusu ujuzi na elimu hiyo muhimu ambayo imepatikana ndani ya nchi bila kuwategemea wageni.